Loading...

Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 16


MTUNZI: MC Short Charles Gwimo

Ilipoishia.........Niliinama kwa aibu kwani hata ile salamu yetu ya kawaidi siku hiyo nilishindwa kuitoa ipasavyo licha ya kuzaliwa na kukulia katika mazingira ya kiimani. Hapo ndipo nilipogundua ya kuwa niko kwenye FUMANIZI LA MAPENZI. Kwa kuwa ilikiwa ni zamu yangu kuwahudumia wenzangu niliungana nao na ibada au kipindi kikaanza huku nikisumbuliwa na harufu kali ya shombo la janaba ambalo nilihisi kuwa mule ndani wote pua zao zimeshaninusa, kumbe sivyo bali ni hofu iliyoambatana na kuathiriwa kisaikolojia na dhambi niliyoivamia kilimbukeni.

Endelea nayo: Niliungana na wenzangu kwenye kipindi cha dini nikiwa mtoa huduma wa siku hiyo. Kwa kuwa sikuwa na maandalizi yoyote, nilikiendesha kipindi kwa uzoefu wangu wa siku zote kwa kuiendesha kipindi kwa kutumia rejea ya kumbukumbu za nyuma nilizowahi kufundishia. Vijana wenzangu walitegemea kupata vitu moto kutoka kwenye kipindi cha siku hiyo, kinyume chake wakaambulia patupu. Kikubwa ambacho walitegemea kukipata kutoka kwangu ni mahubiri ambayo yanalenga kuwakosoa vijana wacha Mungu waliojiingiza kwenye disko la “welcome form one”, kitendo ambacho ni kinyume na malezi ya kikundi hapo shuleni kwa mujibu wa muongozo wetu. Mahubiri yangu yaliwatetea wahanga wote waliosemekana kuvunja utaratibu huo kwa kuingia kwenye muziki na kufanya yale yamchukizayo Mwenyezi Mungu. Kwa kuwa nilijifahamu moyoni kuwa mimi ni mmoja wa wadhambi niliyejivika ngozi ya mwanakondoo ilihali mbwa mwitu mkali, niliwatetea wenzangu kwa kifungu hiki cha maneno, “…wenye afya hawana haja na tabibu isipokuwa wgonjwa tu…….sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.”

********

Nilivielezea vifungu hivyo kwa hisisa kali sana kama vile naongea na Yahwe moja kwa moja. Niliwahutubu wenzangu kwa kuwaambia kuwa, hauwezi kumjua mdhambi bila kuwa karibu naye na hapo ndipo utakapojua mbinu za kumuokoa dhambini kwani maandiko yanasema “kimuingiacho mtu sio najisi, bali kile kimtokacho mtu ndio najisi, kwa maana ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivu, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, matukano, kiburi, na upumbavu….” Haya yote huwa hayatoki nje ya mtu bali hutoka ndani ya mtu na kuwa najisi na machukizo mbele za mwenyezi Mungu na jamii kwa ujumla.

Utulivu ulikuwa ni wakutosha kuliko siku zote ambazo niliwahi kuhudumu kama muhubiri au mtoa neno. Nilishuka gombo mpaka machozi yakaanza kunilenga lenga huku maneno yakizidi kunitoka kinywani mithili ya mtu aliyeshukiwa na upako kutoka kwa roho mtakatifu. Ndugu msomaji wangu, siku hiyo nilitia fora sana hadi sasa ninapokusimulia kisa hiki, sijui nguvu ile ya kuyatoa mahubiri yale ilikuwa ni ya nani, kati ya Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na dunia na Ibilisi msababisha raha ya muda mfupi na karaha pamoja na mateso ya kudumu. Nasema hivyo kwa sababu, ni muda uliokuwa haujazidi hata masaa sita nilikuwa kwenye unajisi mkubwa maeneo ya Kibirizi kwa kufanya uzinzi na Fauzia kwa matamanio ya kutoka moyoni. Hapo ndipo wahubiri wengi wenye tabia kama zangu huwa wanajiwekea kinga ya maneno kama vile “…yashikeni niwafundishayo wala msiangalie matendo yangu” hasa pale wanapojigundua kwamba matendo waliyofanya gizani yameonekana mwangani na hivyo hayana budi kukemewa. Nilihitimisha mahubiri kwa kupigiwa makofi mengi na mbinja mfululizo mpaka pale mwenyekiti alipowatuliza washiriki wote kwa salamu yetu ya kila siku kwa mujibu wa imani yetu.


********

Mwenyekiti alisimama akanipongeza kwa maneno matamu huku akisema, “Mwenyezi Mungu ni wa ajabu sana, wakati ibilisi na kundi lake wako mawindoni, yeye huweza kumtumia mtu mmoja tu kuwasambaratisha kundi zima. Ukweili huu unajidhihirisha kwa mtumishi David ambaye Mungu anamtumia kama chombo cha kulitangazia neno lake na daraja la kuwaunganishia watu wake ili wasipotee.” Mwenyekiti aliendelea, “Mafundisho ya David ya leo yamemgusa kila mtu aliyemo humu ndani kwa kupokea Baraka tofauti tofauti……, binafsi kama Mwenyekiti nimesuuzika moyo sana kwa mafundisho ya leo na ninapenda kuwatamkia kuwa, kwa mujibu wa mafundisho ya mtumishi wetu David, ninazibatilisha adhabu za vitengo kwa wale wote walioenda kinyume na utaratibu wetu wa kushiriki maovu ya kumchukiza muumba, kikubwa ninachowaomba ni kutoyarudia hayo machukizo”. Alipomalizia kutamka maneno hayo, alipokelewa na neno Ameeee! Kutoka kwa wanakikundi wote.

Kipindi kilifungwa mnamo saa tatu na nusu usiku kwa Baraka kutoka kwenye kundi la wanamaombi ambao tuliwahusudu katika eneo hilo ingawa wengine walikuwa kama chaja ya kobe isiyochagua simu ya kuchaji. Hapa ninamaanisha wale ambao kwenye kitabu cha ufunuo wa Yohana wapo kwenye makundi yote ambayo si baridi wala moto bali uvuguvugu na hao ndiyo watakaotapikwa watoke kinywani kwani maneno yao yanakinzana na matendo yao. Miongoni mwa watu hao ni pamoja na mimi niliyekumbwa na FUMANIZI LA MAPENZI tena ya mwendokasi huku nikijifanya mcha Mungu wa hali ya juu. Ndugu msomaji wangu, kulingana na mambo ambayo tulikuwa tukiyafanya kinyume na utaratibu wa imani zetu hakika tulikuwa kama MAFARISAYO na MASADUKAYO ambao ni wanafiki juu ya imani kwa kumuheshimu Mungu wao kwa midomo tu ila mioyo yao iko mbali naye.


********

Tulitawanyika kuelekea mabwenini ili kwenda kupumzika tayari kwa kuipokea siku mpya ya masomo, yaani Jumatatu. Nilimkuta rafiki yangu Mood akipunga upepo chini ya mti wa mlimao kwenye maeneo yetu ya kupumzika akiwa amenisubiria. Hatukupoteza muda bali tulijiandalia chakula tulichokuwa tumehifadhiwa na mmoja wa wanabweni wenzetu ambaye hakubahatika kutuona kwenye foleni ya chakula hivyo akaamua kutuchukulia ‘shea’ yetu kwa kisingizio kuwa tuko kwenye vikao vya kidini ukizingatia tunavyoheshimika kutokana na uchaji Mungu wetu wa kinafiki unaoonekana kama lulu kwa wale wasiojua upande wa pili wa maisha yetu. Tulimpongeza sana kijana huyo kwani bila yeye tungelalia ngumi na usiku kuuona kama moja ya kero muhimu kwetu kwa siku hiyo.


********

Tuliingia kulala huku tafakuri yangu ikiwa kinyume na kile kilichonisababisha kuwa pale shuleni. Nikiwa kitandani mwangu, mawazo yalinichukua kwa kunitembeza kona mbalimbali za mahaba kwa kunikutanisha na vimwana mbalimbali ambao wengine kwangu niliwaona kama michoro ya kubuni na wengine sikuamini kama wapo kwenye dunia hii ya Mola. Usingizi ulinipitia bila aina yoyote ya njozi mpaka pale niliposhtuliwa na kelele za wanafunzi wenzangu waliokuwa kwenye harakati za kuelekea katika maeneo yao ya kazi, na hapo ndipo nilipogundua kuwa siku niliyokuwa nikijivunia kuiita leo imebadilika jina na kuitwa jana na leo yangu imekuwa Jumatatu.

====>>Itaendelea Ijumaa...

Usiikose SEHEMU YA 17>>> ya Riwaya hii ifikapo Ijumaa ya wiki hii, na utaipata hapa Zero Degree pekee.
Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 16 Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 16 Reviewed by Zero Degree on 7/24/2017 08:46:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.