Loading...

Maalim Seif na mbinu mpya kumkabili Profesa Lipumba

Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kwa niaba ya wabunge wenzake wa Chama cha CUF, mjini Dodoma hivi karibuni
Tangu Chama cha Wananchi (CUF) kiingie katika mgogoro wa uongozi, mambo tofauti yamekuwa yakijitokeza hali inayozidisha sintofahamu kwa wanachama na Watanzania kwa ujumla kuhusu hatima ya chama hicho.

Mgogoro huo unatokana na hatua ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu mwaka 2015 na baada ya mwaka mmoja akatengua uamuzi wake. 

Wakati ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikiendelea kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa chama hicho, majaliwa kwa upande wa pili ulio chini ya katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad yamebaki yakitegemea zaidi mahakama.

Ni kwa njia hiyo, mtanzuko uliopo utaondolewa baada ya kesi za kupinga uamuzi wa msajili na mabadiliko ya bodi ya wadhamini yaliyofanywa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) ukipatiwa ufumbuzi.

Pamoja na hatua hiyo ya Maalim Seif kupingana na uamuzi wa Rita akisema imesajiliwa kinyume cha utaratibu pamoja na hatua zote za msajili wa vyama, bado ana silaha nyingine ya msaada ni wafuasi na viongozi waliopo nyuma yake.

Katika matumizi ya ‘silaha’ hiyo, kwa siku za karibuni makundi mbalimbali ya viongozi wa chama, wabunge, madiwani na makatibu wa kanda yamekuwa yakiibuka na kutoa matamko ya kumpinga mwenyekiti na kujitanabahisha kuwa upambe wa Maalim Seif.

Hiyo ni ishara kuwa licha ya nguvu kubwa aliyonayo Profesa Lipumba upande wa vyombo vya Serikali, ana kazi ngumu kushawishi uungwaji mkono ndani ya chama.

Hata hivyo, hapana shaka kwamba mgogoro huo umesababisha chama hicho kugawanyika katika pande mbili – unaomuunga mkono Profesa Lipumba na wa Maalim Seif, ingawa viongozi hao wa juu kwa nyakati tofauti wamekuwa wakisema hakuna CUF mbili.

Kwa halisi ilivyo sasa, CUF ya Profesa Lipumba inashikilia ofisi za chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam wakati upande wa Maalim Seif unashikilia ofisi za Makao Makuu zilizopo Mtendeni, Zanzibar, huku upande wa Bara akifanyia shughuli zake katika ofisi mpya za Magomeni, Dar es Salaam zilizoandaliwa na wabunge wa chama hizo.

Kati ya wabunge 42 wa chama hicho; wawili akiwamo mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya na Maftaha Nachuma wa Mtwara Mjini ndiyo wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.

Sakaya alinukuliwa na gazeti hili akisema ofisi ya Magomeni ipo kinyume cha Katiba ya CUF inayoeleza kuwa kutakuwa na ofisi mbili; ya Buguruni na ya Zanzibar.

Kuhusu mgawanyiko wa viongozi kila upande umesaliwa na wanaounga mkono, na wakati mwingine kuteua makaimu katibu na wakurugenzi ili kuimarisha safu zao.

Profesa Lipumba aliteua baadhi ya viongozi wakurugenzi na wajumbe wa bodi, akiwamo Sakaya aliyeteuliwa kuwa kaimu katibu mkuu kufanya kazi za Maalim Seif ambaye alisema hafiki ofisini.

Wakati Profesa Lipumba akiteua viongozi hao, Maalim Seif aliwasimamisha uanachama mwenyekiti huyo na baadhi ya viongozi wenzake akiwamo Sakaya kwa madai ya kukiuka taratibu za chama hicho.

Mbinu za Maalim

Wingi wa wabunge wa CUF umeendelea kumpa nguvu Maalim Seif. Wamegharamia ofisi ya Magomeni na kuusaidia upande huo katika uungwaji mkono. Wabunge hao waliwahi kukutoa tamko la kwenda Buguruni kufanya usafi ofisini, hatua iliyozuiwa na polisi kwa maelezo kwamba ingesababisha vurugu.

Hata juzi, wengi wao walifika mahakamani kufuatilia kesi mbalimbali za chama.

Ukiacha kundi hilo, wapo madiwani 18 kati ya 21 wa CUF katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao nao hivi karibuni walitoa tamko la kumuunga mkono Maalim Seif, ukiacha watatu waliopo upande wa mwenyekiti Lipumba.

Akitoa tamko hilo kwa niaba ya wenzake aliokuwa nao, diwani wa Kiwalani, Mussa Kafana anasema wanamuunga mkono na wapo bega kwa bega Maalim Seif.

Anasema katibu mkuu alikuwa sahihi kueleza umma sababu za kutokubaliana na hatua ya Rita baada ya kusajili majina ya bodi ya wadhamini yaliyowasilishwa na Profesa Lipumba.

Kafana anasema wanaazimia kuipinga Rita mbele ya Mahakama Kuu kwa kufungua kesi dhidi yake kwa mujibu wa kifungu cha 26 kwa kukiuka taratibu za Sheria za Wadhamini.

Wakati madiwani na wabunge wengi wakitangaza kumuunga mkono Maalim Seif, hivi karibuni pia waliibuka makatibu wa chama hicho kutoka kanda sita ambao pia walitoa tamko la kumuunga katibu mkuu huyo kuwa bado wanalitambua Baraza Kuu la Uongozi Taifa lililochaguliwa Juni 2014.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake aliokuwa nao mjini Dodoma, Ally Darema alimtaka Profesa Lipumba kuicha ofisi ya Buguruni na kuomba ajira kwa msajili wa vyama vya siasa na kwamba akiendelea kukaidi wanachama wataichukua ofisi hiyo.

Hata hivyo, kujitokeza kwa viongozi hao mfululizo kunaelezwa na Sakaya kuwa ni kutapatapa na kutafuta huruma ya chama, lakini upande wao unaendelea na msimamo wake kufuata katiba ya chama hicho.

“Labda nikwambie, wale wanaojiita makatibu wa kanda si lolote si chochote, wamekusanywa na mchakato mzima umeandaliwa na watu kutoka Dar es Salaam hasa wilaya ya Ilala,” anasema Sakaya na kuongeza kuwa; 

“Katiba ya CUF haina kipengele kinachoeleza kuna katibu wa kanda, sasa wao mamlaka wameitoa wapi? Nilifuatilia mwanzo mwisho mkutano na jioni mmoja wao alinipigia simu na kunieleza kuwa walikusanywa na kutoa tamko kwa miadi ya kupewa Sh200,000 kwa kila mmoja kutokana na hali ngumu ya maisha.” 

Alifafanua kwamba, baada ya viongozi hao kukusanywa wote walinyang’anywa simu na walitakiwa kufuata maelekezo kutoka kwa watu wa CUF wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao walishirikiana na mbunge mmoja kutoka Pemba.

Sakaya ambaye ni naibu katibu mkuu wa chama hicho (Bara), anasema watamchukulia hatua katibu wa Wilaya ya Babati ambaye alikuwa kinara katika mchakato huo ili iwe fundisho kwa wengine.

“Hizi ndizo dalili za kifo cha mende, Seif (Maalim) ndiye anayekivuruga chama kutokana na mpango wake wa kukihujumu. Narudia CUF itaendelea kusimamia katiba,” anasema Sakaya. 

Hata hivyo, Sakaya anapingwa na mkurugenzi wa habari, uenezi na uhusiano kwa umma, upande wa Maalim Seif, Salim Bimani anayesema hatua ya viongozi hao kumuunga mkono Maalim Seif inaonyesha CUF ni taasisi na kwamba viongozi na wanachama wanasimamia Katiba.

“Chama ni vikao, yaani Baraza Kuu, Kamati ya Utendaji na mkutano ndiyo anavyovitekeleza Maalim Seif, lakini upande mwingine hawafanyi hivyo ndiyo maana viongozi wanaojua katiba ya CUF wanaangalia upande upi una umuhimu,” anasema Bimani. 

Anasema viongozi na wanachama wa CUF wanafahamu taratibu za chama hicho na kwamba hawezi kuyumbishwa na upande usiofuata kanuni, katiba ambao wana lengo la kukivuruga na kukidhoofisha chama hicho cha wananchi.

Bimani anasema kitendo kilichofanywa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Profesa Lipumba ni kinyume cha utaratibu na katiba ya chama hicho haina kipengele kinachosema mtu akijiuzulu anarudi katika wadhifa wake.

Kuhusu madai ya kuwakusanya makatibu wa kanda kutoa tamko la kumuunga mkono Maalim Seif, Bimani anasema hakuna watu waliokusanywa bali viongozi hao walifuata taratibu zote za kufanya mkutano na kutoa ya moyoni kuhusu mwenendo wa CUF.

“Sakaya amesimamishwa CUF, vilevile hakitambui vizuri chama, wale viongozi hawajakusanywa kama anavyodhani. Naomba asipoteze muda wake yeye yupo peke kama ng’ombe asiye na pembe, kama anaona tumewakusanya basi na yeye awakusanye anaowajua ili watoe tamko la kumuunga mkono Profesa Lipumba,” anasema Bimani. Anasema anamshangaa Sakaya kwa hatua yake ya kuwageuka na kuiponda Ukawa wakati imemsaidia sana kushinda ubunge wa Kaliua na miaka yote wanashiriki lakini hawaambulii kitu, lakini mwaka juzi Ukawa walifanya uamuzi mgumu. 

“CUF peke yetu hatuwezi kushinda Kaliua, ndiyo maana kuna madiwani wengi wa Chadema kuliko wa CUF katika jimbo lile lakini mwenzetu halioni hili badala ya anatushambulia,” anasema Bimani. 

Hata hivyo, Bimani anasema CUF haina tabia ya kutoa fedha kwa viongozi ili wamuunge mkono mtu fulani na kwamba upande wa Profesa Lipumba ndiyo wenye tabia hizo.

Wengine wanawasemaje?

Wakati CUF wakijibishana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala anasema hatua ya wabunge, madiwani na makatibu kujitokeza hadharani na kumuunga mkono Maalim Seif kuhusu mustakabali wa chama hicho inaashiria wanaujua ukweli kuhusu mgogoro uliopo.

“Jambo feki linajulikana, yule bwana (Profesa Lipumba) alishajiuzulu. Lakini akalazimisha kurudi kwa mgongo wa watu fulani, sasa kwa viongozi na wanachama wanaojua ukweli lazima waangalie upande upi wa kuunga mkono,” anasema. 

Profesa Mpangala anasema viongozi wanaomuunga mkono Maalim Seif wanaona mkakati wa Profesa Lipumba unataka kukidhoofisha chama hicho kilichopo katika Ukawa unaojumuisha vyama vingine vya Chadema, NCCR –Mageuzi na NLD.

Anawashauri viongozi wanaomuunga mkono Maalim Seif kuendelea na msimamo huo na kutokata tamaa ili kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ili chama kifanye shughuli zake kwa ufanisi.

Kinyume na mawazo ya Profesa Mpangala. Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda anasema hatua ya viongozi hao kumuunga mkono Maalim Seif inaonyesha mgawanyiko wa wazi ulipo katika chama hicho kikongwe.

“Kuna upande unaodaiwa kuchochea mgogoro na upande mwingine unadai una uhalali. Hii inatuonyesha picha halisi iliyopo katika CUF. Kila mmoja ana nguvu sehemu yake; Profesa Lipumba Bara na Maalim Seif Zanzibar. 

Mhadhiri huyo anahitimisha kwa kusema: “2020 inakuja kwa kasi sana ili chama kisimame na kushiriki uchaguzi mkuu kwa ufanisi lazima kiachane mgogoro na badala viongozi kuwa kitu kimoja kwa mustakabali wa chama chao.”

Source: Mwananchi
Maalim Seif na mbinu mpya kumkabili Profesa Lipumba Maalim Seif na mbinu mpya kumkabili Profesa Lipumba Reviewed by Zero Degree on 7/08/2017 01:53:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.