Loading...

Rais Magufuli amgeuzia kibao aliyemuita David Kafulila 'tumbili'


RAIS John Magufuli jana alimpongeza aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila kwa hatua yake ya kuibua kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya akaunti ya Tegeta Escrow inayohusu Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Kafulila ambaye kwa sasa amehamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliibua kashfa hiyo katika Bunge la bajeti la mwaka 2013.

Wafanyabiashara wawili, Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira wamesomewa mashtaka 12 ikiwamo ya kugushi, utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya dola za Marekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4 kwa serikali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mapema mwezi huu kuhusiana na akaunti hiyo.

Rugemalira ni Mkurugenzi wa VIP Engineering na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, na Sethi ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP).

Kafulila alilieleza Bunge kuwa zaidi ya Sh. bilioni 200 zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa dhumuni la kuweka fedha wakati wa mgogoro kati ya Tanesco na IPTL, zilichotwa kifisadi na baadhi ya viongozi.

Kufuatia hatua hiyo, Bunge lilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya ukaguzi na uchunguzi wa fedha hizo.

Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji wilayani Uvinza mkoa wa Kigoma, Rais Magufuli alisema Kafulila anapaswa kupongeza kwa hatua yake ya kuwapigania Watanzania wasiibiwe kiasi hicho cha fedha.

"Nitakuwa mnafiki nikiondoka hapa bila ya kumpongeza aliyekuwa Mbunge wa hapa... Kafulila," alisema Rais Magufuli. "Ni mzalendo." 

"Alilizungumzia sana suala la IPTL na wizi mkubwa uliokuwa unafanywa na baadhi ya watendaji wa serikali. 

"Walimpinga, lakini siku zote ukweli utabaki kuwa ukweli, ukweli unaweza kucheleweshwa, ukweli unaweza kugeuzwa, lakini ukweli siku zote utabaki kuwa ukweli." 

Rais Magufuli aliwaomba wananchi wa uvinza kumfikishia salamu zake kwa Kafulila na kuwaeleza kuwa salamu zake zinatoka moyoni, kwa kutetea haki za Watanzania wasiendelee kuibiwa.

"Sitaki niwe mnafiki, kwa sababu nitaenda kuhukumiwa kwa kutompongeza Kafulila," alisema Rais Magufuli.

"Sitaki niwe na dhambi hiyo itakayonipeleka motoni. 

"Kafulila wewe ni hodari, ulisimamia wizi wa IPTL ambao ni wizi wa ajabu, wengine wakamtisha kumpeleka mahakamani, wakamtukana, wengine wakamwita tumbili. 

"Sasa tumbili amefanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania." 

Kafulila aliitwa tumbili na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema Juni 26, 2014.

Kabla ya kutoa kauli hiyo, Werema alikuwa akitoa ufafanuzi wa mwongozo ulioombwa na Kafulila, kuhusu fedha zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT), ambazo zililipwa kwa PAP inayomiliki mitambo ya IPTL.

Werema alisema fedha hizo si za Serikali kama inavyodaiwa na Kafulila, kwa kuwa fedha za serikali hazikai katika akaunti hiyo.

Wakati akizungumza, Werema alitumia mfano wa kabila la Wanyankole aliosema wana usemi unaosema kwamba 'tumbili hawezi kuamua kesi ya msituni'.

Kabla ya kufafanua maana ya msemo huo, Kafulila bila kuwasha kipaza sauti, alikuwa akipiga kelele kumuita Werema kuwa ni mtuhumiwa, hivyo atangaze maslahi yake.

“Naomba nisikilize, hata kama ni mtuhumiwa, nina fursa ya kusikilizwa… nisikilize wewe tumbili,” alisema Werema. 

Lakini Rais Magufuli alisema jana kuwa waliompinga Kafulila wakati huo wao ndiyo matumbili.

"Wao ndiyo matumbili," alisema Magufuli. 

"Kafulila nakupongeza kwa dhati bila ya unafiki. 

"Japokuwa upo katika chama kingine, kwa hili nitakupongeza kwa dhati maisha yangu yote.
"Kafulila oyee." 

Aliongeza kuwa nchi ilikosa viongozi wazalendo wa kuwatetea Watanzania, na kwamba viongozi wengi waliochaguliwa walikuwa wakijali maslahi yao binafsi.

Akizungumza na Nipashe kuhusu pongezi za Ikulu za jana, Kafulila alisema amefarijika kwa hatua ya Rais Magufuli kuguswa na kutambua mchango wake.

"Kwenye vita hii hakuna chama, niliteseka sana ndani na nje ya jimbo kutokana na vita hii, zilifanyika kila hila na njama, lakini namshukuru Mungu kuwa upande wangu hata nimebaki hai," alisema Kafulila. 

"Ukweli nimefarijika sana kuona mkuu wa nchi amelizungumzia jambo hili jimboni kwa wananchi walionipenda sana amezungumzia kwa hisia na uzito wa kutosha," alisema Kafulila. 

Kafulila alisema kwenye vita ya ufisadi nchini anamuunga mkono Rais Magufuli na kumshauri kuwa ajenge mfumo na taasisi imara za uchunguzi na uendeshaji mashtaka katika eneo hilo ili kuhakikisha vita hiyo inakuwa ya mafanikio makubwa.

Alisema tamaa yake ni kuona ufisadi wa IPTL na Escrow hakuna jiwe linasalia juu ya jiwe, ikiwamo waliobeba mabilioni kwa lumbesa katika benki ya StanBick.
Rais Magufuli amgeuzia kibao aliyemuita David Kafulila 'tumbili' Rais Magufuli amgeuzia kibao aliyemuita David Kafulila 'tumbili' Reviewed by Zero Degree on 7/24/2017 09:22:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.