Loading...

Diwani apandishwa kizimbani kwa kujifanya Usalama wa Taifa


DIWANI wa CCM Kata ya Sambasha, Lengai ole Sabaya (30), ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) mkoa wa Arusha, amepanda kizimbani kwa makosa mawili, likiwamo la kujifanya mtumishi wa umma wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), kosa ambalo amewahi kufutiwa mara tatu.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Sabaya jana alidaiwa pia kughushi kitambulisho cha Usalama wa Taifa na kuweka picha yake.

Alifikishwa mahakamani hapo akitokea polisi alikokuwa amewekwa mahabusu tangu juzi.

Akimsomea mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nestory Mwankuga, Wakili wa Serikali Penina Joachim alidai kosa la kwanza linalomkabili Sabaya ni la kujifanya mtumishi wa umma.

Joachim alifafanua kwamba Mei 18, mwaka huu, akiwa katika Hoteli ya Skyway iliyoko eneo la Makao Mapya jijini hapa, alijifanya kuwa mwajiriwa wa TISS.

Alidai kosa la pili katika siku isiyofahamika wala tarehe lakini mwaka huu, alighushi nyaraka za kitambulisho cha Usalama wa Taifa chenye picha yake na kutumia namba Saturday Code Eagle 3 chenye namba MT. 86117

Hata hivyo, Sabaya alikana makosa hayo na ndipo Wakili wa Serikali Penina aliposema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na dhamana ya mshtakiwa iko wazi.

Wakili wa utetezi, Edna Mndema, alimwomba hakimu kuweka kwenye kumbukumbu zake kuwa ni mara ya nne mteja wake anafikishwa katika mahakama hiyo kwa kosa hilo hilo.

Hakimu Mwankuga alisema kwa kuwa dhamana iko wazi, anampa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, ikiwamo kutia saini hati ya dhamana ya Sh. milioni tatu kwa kila mdhamini.

Sabaya aliachiwa baada ya kutimiza masharti hayo na kutakiwa kufika mahakamani kila tarehe yake kesi ambayo imeahirishwa hadi Agosti 30.
Diwani apandishwa kizimbani kwa kujifanya Usalama wa Taifa Diwani apandishwa kizimbani kwa kujifanya Usalama wa Taifa Reviewed by Zero Degree on 8/12/2017 09:55:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.