Loading...

Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 20


MTUNZI: MC Short Charles Gwimo

Ilipoishia.........Nilimsogelea kisha tukaanza kunyonyana ndimi zetu ili tuagane kwa kuepuka kukutwa na wanafunzi waliokuwa na shida kwa madamu. Zoezi lilipokuwa linaelekea kufikia tamati, tulishituliwa kwa sauti ya mlango, ngo! ngo! ngo! ngooo! hodi! hodi! nilijichomoa kutoka mikononi mwa madam na kuchanja mbuga hadi chumba cha huduma ya kwanza ili nijifiche kuepuka kufumaniwa na wanafunzi au walimu ndani ya FUMANIZI LA MAPENZI kati yangu na Madam Linda.

Mapigo ya moyo yalikuwa yanakimbia mithili ya mwanariadha wa mbio za nyika. Nilijibanza kwenye meza kubwa iliyokuwa imehifadhi madawa ya huduma ya wanza lengo likiwa ni kulikwepa fumanizi la aibu kati yangu na madam Linda. Huku nikiwa ninahema kwa taratibu kwa kuogopa ili uwepo wangu usijuliane ndani ya ofisi nyeti ambayo ni mahususi kwa faragha za wanafunzi wa jinsia ya kike, masikio yangu yalikua wazi kama kaunta ya polisi yakisubiri kuupokea umbea kutoka chumba namba moja ambacho ndio ofisi ya Idara ya somo la elimu ya viumbe. Kwa mbali nilisikia sauti ya madam ikimkaribisha mgeni aliyekuwa akitugongea hodi. nilijisogeza taratibu karibu na mlango ili niweze kumtambua mgeni aliyekaribishwa mle ofisini. Hamadi yangu! Nilipata mshituko wa ghafla mara baada ya macho yangu kumshuhudia mwalimu aliyeogopeka shule nzima kwa ucharazaji wa viboko kwa wanafunzi. Huyu hakuwa mwingine bali alijulikana kwa jina la Mwalimu Kishoto aliyehusika na Idara ya nidhamu na taaluma.

**********

Nilitetemeka mpaka nikahisi tumbo la kuendesha linaninyemelea, kwani nilihisi vitu kama maji maji vikichanja mbuga kupitia kwenye mfereji wa mwaranda. Nilisikia sauti ya madam ikimkaribisha mwalimu Kishoto kwa ukarimu na ucheshi mkubwa ingiwa binafsi moyoni nilishajua uchangamfu hule ulisababishwa na nini. “Mwalimu Mashoto, karibu sana ofisini kwangu kwa mchana huu. Unajua tulishawazoea nyie walimu wa taaluma wote kuwa hampendi kutoka ofisini kwenu mpaka linapotokea suala la kitaaluma kama vile uandaaji na usimamizi wa mitihani .” Madam alitiririka maneno kama cherehani ya kudarizi akimnyima muda wa kuongea mgeni huyo katika ofisi yake. “Eeeh! Leta habari mpya basi wangu wa taaluma, kuna nini nipokee kwa mikono miwili?” Nilimsikia mwalimu Kishoto akijikoholesha kikohozi kikavu kama vile mvutaji wa bangi aliyepaliwa na moshi mzito wa bangi ile yenye asili ya mgando. Kupitia kwenye upenyo ulikokuwa kwenye nyufa za mlango, nilimuona mwalimu Kishoto akiwa mbali sana kimtazamo kwani moja kwa moja alishindwa kuelezea kinagaubaga jambo lililomfikisha kwenye ofisi ya madam. Alikuwa akiuma uma mdomo wa chini na juu huku akionekana kama vile mtu aliyegubikwa na aibu ukweni.


**********

Hatimaye mwalimu Kishoto alipata gia ya kuanzia, “Samahani madam kwa kukufanyia ziara ya ghafla ofisini mwako, sina maneno ya ugeni mdomoni mwangu zaidi ya ukasuku wangu wa siku zote uliouzoea kusikia ambao kwa sasa umekuwa kama wimbo wa kupandishia bendera ya taifa.” Kabla ya kuendelea kwa kile alichokifuata mle ofisini aliomba radhi ili aulize swali, “Madam Linda, nilipofika ofisini kwako nilikuta mlango ukiwa umefungwa kwa funguo, hivi hakuna mtu yoyote chumba cha pili ambaye anaweza kunivurugia lengo la ujio wangu? Yaani namaanisha hakuna mtoto wa kike aliyekuja kufanyiwa huduma ya kwanza ofisini kwako kwani ofisi imetawaliwa na hewa nzito mithili ya masazo ya pedi jambo ambalo limenifanya nisite kukuulizia.” Madam aliangua kicheko cha nguvu, “Kwe kwe kwe kwee!” Mpaka mwalimu Kishoto akasinyaa huko uso ukiwa umeparama.


**********

Aliporidhika kwa kicheko chake, madam alimpoza mgeni wake ili ajisikie kuwa yuko huru ndani ya ofisi hiyo, “Nisikilize mwalimu Kishoto, kwa maneno uliyoniuliza haukukosea kabisa kwani nilikuwa na kazi nzito humu ndani ya kuwapa huduma ya kwanza mabinti wanne waliokuwa katika mizunguko yao ya mwezi pasina kujijali kiafya kwa kukaa na pedi kwa muda mrefu bila ya kuzibadilisha. Kwa kweli tuna haja ya kuongeza walimu wa kike kwa ajili ya kulikabili suala hili. Kwa wengine huwa mizunguko yao huambatana na kuumwa huku wakikabiliwa na maumivu makali ya tumbo kama hawa niliokuwa nao humu ndani. Baada ya hao mabinti kuondoka, nami niligutushwa na kuloana kwa nguo yangu ya ndani na nilipojichunguza tarehe hazikunidanganya kwani nilikuwa tayari nimeshampeleka kuku kibla, …..kwaiyo kuchelewa kwangu kukufungulia nilikuwa kwenye kujiboresha.” Huyo ndiye madam Linda mtu niliyemhusudu kama dada na mwalimu wangu licha ya kuwa mmoja wa walezi wangu wa kiimani. Kwa uongo alioupanga, nisingekuwepo mazingira ya tukio nisingemkubalia mtu kwa yoyote kama simulizi hii inamhusu madam Linda zaidi ya kumchafua jina na hadhi yake ndani ya jamii.


**********

Mwalimu kishoto alimuomba msamaha madam Linda kwa kumkatisha kwa zoezi hilo lisilohitaji uchafu abadani. Madam alimsamehe kisha Kishoto akaendelea, “Madam Linda, ujio wangu kwako si mpya kama nilivyokuambia toka awali. Bado ninaendelea kukufuatilia ili uwe mke wangu wa ndoa endapo tu utakubali kunipokea kwa mikono miwili ndani ya nafsi yako na kuniweka kwenye moja ya kurasa za upendo zilizomo chini ya uvungu wa moyo wako. Ninakuahidi endapo utanikubalia ombi langu la kuwa mchumba wako, mshahara wa mwezi huu nitakukabidhi wote ili ujinunulie samani zote za ndani na vitu vingine uvipendavyo.” Ndugu msomaji wangu, mapenzi yana nguvu kuzidi hata ‘burudoza’ kwani kwa muda wote huo wa maongezi baina ya Madam Linda na mwalimu kishoto, mwalimu huyo wa kiume alikuwa ameyapiga magoti yake kwa hiari huku akibembeleza kupendwa.


**********

Nikiwa bado nimejificha chumba cha huduma ya kwanza, amani ya moyo ilirudi kuwa ya kawaida baada ya kugundua kumbe hata mgeni aliyeko mle ofisini naye keshafumaniwa na mapenzi kibaya zaidi ameshafikia hatua ya kuumilikisha mshahara wake wote wa mwezi. Ingawa nilikuwa na furaha ya kutosha moyoni baada ya kugundua kuwa mimi na mwalimu Kishoto wote tu wahanga wa mapenzi ingawa kidonda cha wivu hakikunibanduka moyoni. Nilipiga moyo konde kwani nilishajiaminisha kwa lolote lile atakalonitendea Madam linda, yaani kupewa huduma wa kwanza au wa mwisho kwa sababu mfuko wangu haukuwa na alama za kusomeka zaidi ya vumbi la ufukara.


**********

Nilishuhudia madam Linda akimnyenyua mwalimu Kishoto aliyeonekana kupooza mithili ya kifaranga cha kuku kinachosubiria nyongo kwa mamaye. Kisha nikasikia sauti ya madam, “Samahani sana mwalimu mwenzangu, kwa leo sina majibu ya moja kwa moja ya kukupa kwani hali yangu ya kike kike ndiyo tatizo kubwa. Nilitamani hata leo ingewezekana nikukubalie ombi lako lakini ninakuomba muda wa siku mbili ili nikupatie majibu yako ambayo yatausuza moyo wako. Lakini pia suala lako litakubaliwa endapo tu utatimiza ahadi yako ya kuninunulia samani za ndani.” Nikiwa mafichoni nilicheka kimoyomoyo kwa kitendo cha mwanaume mwenzangu kupewa masharti magumu kama vile ya nchi wafadhili huku nikisahau kuwa matatizo ya wanaume wote duniani katika suala la mapenzi hufanana ingawa hayalingani.


**********

Madam na mwalimu Kishoto waliagana kwa mabusu ya kinafiki huku nikiujua ukweli wa upande mmoja na kusahau kuwa, “Kilichompata ngwena na kiboko ndicho.” Waliagana kwa mashamsham kwa kurushiana mabusu ya hewani huku madam akuizidisha uongo kwa kumwambia, “Ningekufikisha mbali ila tu pedi sijaibana vizuri. Tutaonana eeh!”

====>>Itaendelea Ijumaa...

Usiikose SEHEMU YA 21>>> ya Riwaya hii ifikapo siku ya Ijumaa wiki hii, na utaipata hapa Zero Degree pekee.
Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 20 Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 20 Reviewed by Zero Degree on 8/07/2017 10:10:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.