Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 23
Ilipoishia.........Hivyo ndivyo maisha ya shule yalivyokuwa enzi hizo za utawala wa mzee ruksa kwa nchi hii ya wadanganyika kwa wanafunzi wa bweni. Hayo ndiyo yaliyokuwa maisha ya wanafunzi tuliokuwa tukisomea shule za sekondari za bweni. Tofauti na madhila hayo ya shule wengi walijipatia ahueni mara baada ya kupata likizo kwani watoto wa kike wa enzi hizo za kipindi cha utawala wa mzee wa ruksa waliwahusudu sana vijana wa kiume walioko masomoni hasa wanapotajiwa kuwa wapenzi.
Endelea nayo: Purukushani za maisha ya shule hazikuwa tofauti sana kimalezi na ubabe kama ilivyo kwa maisha ya magereza kwa mienendo ya kunyanyasana. Manyanyaso makubwa yalifanywa na viongozi wa shule yaani viranja kwa wanaowaongoza kuanzia kwenye malezi hadi chakula. Ni wababe tu ndiyo waliofaidi maisha halisi ya shule kama nilivyokujuza hapo awali. Kwa upande wangu nilijivunia kuwa na nyota ya kupendwa kama hela jambo ambalo lilikuwa kama ulinzi wangu wa asili niliotunukiwa na mola kupitia tumbo la mama yangu mzazi mke halali wa mzee Sikitiko ingawa alikuwa na mitara. Kutokana na kupendwa na jamii ya wengi hapo shuleni, madhila kama hayo niliyasikilizia hewani tena kwa kusimuliwa kama moja ya visasili au hadithi za mivigha kama sio soga.
Ingawa nilibahatika kuwa na nyota ya kupendwa na wengi katika mazingira ya shule, kupendwa huko hakukunifanya nibweteke zaidi ya kujikita kwenye juhudi za masomo. Nilisitisha zoezi la mapenzi kwa muda kwa kuepuka kina madam Linda na wengine wenye muonekano wake ili nijikite kwenye usomaji wa kiwango cha juu kwa lengo la kutetea uwezo wangu wa darasani tofauti na mapenzi niliyoyalimbukia kwa pupa bila kufuata mila na desturi kwa takribani wiki nzima nilijikita kwenye zoezi hilo la usomaji jambo ambalo lilinifanya niwe adimu kwa marafiki zangu wengi wa kiume na kike akiwemo Fauzia. Kwa kuwa nilikuwa na ‘pocket money’ yakutosha niliyozawadiwa na madam, kiyendo cha kupanga foleni kwenye msosi sikukihusudu sana zaidi ya kuwatuma marafiki zangu kunichukulia ugali pasina mboga kwani mboga nilizinunua kwa wauzaji wadogo wadogo wa vyakula pale shuleni maarufu kama wauza mboga za “miungo” yaani mboga mbadala tofauti na ile tunayopikiwa shuleni yaani ‘full suit’, namaanisha ugali kwa maharage kila kukicha.
Mitihani ilifanyika kwa mfululizo wa wiki mbili kutokana na michepuo ya masomo husika. Kwa sisi wanafunzi wa vidato vya chini tulimaliza mapema mitihani yetu tofauti na wenzetu wa kidato cha tano na cha sita. Kwa kuwa tulimaliza mitihani yetu mapema tofauti na wenzetu, muda mwingi tuliutumia kwenye kufanya usafi wa mazingira na muda mwingine kushinda kwenye fukwe za ziwa Tanganyika tukibarizi na kupunga upepo bila kusahau kubadilisha mitazamo misimamo ya kimaisha. Kumalizika kwa mitihani kulinirudisha kwenye fikra za mahusiano tena kama awali kwa kasi ya ajabu huku nikimuweka madam Linda mtimani mwangu kuliko hata Fauzia tuliyeendana kwa umri. Nilijilazimisha kwa fikra na hali kuwatoa hao wote moyoni mwangu ili niyaepuke madhila ya mapenzi katika umri mdogo lakini shetani aliyazidi mawazo yangu kwa kunirudisha zaidi kwenye fikra za mahusiano ya tendo la ndoa.
Hatimaye muda wa kufunga shule uliwadia kwa wanafunzi wote kuwa na mshawasha wa kujua matokeo ya mtihani na mienendo mizima ya kimaadili. Kila mwanafunzi alikuwa na wasiwasi wa kupokea ripoti na taarifa kwani ilisadikika kuwa mara nyingi kutoonekana kwa wanafunzi hasa uanzapo muhula wa pili ulitokana na yale yaliyotolewa kipindi cha kufunga shule. Taarifa kama hizo zilikuwa hazitolewi moja kwa moja kwa wanafunzi bali zilitolewa kama tetesi na hatimaye taarifa rasmi zilitumwa moja kwa moja kwa mzazi au mlezi wa mwanafunzi husika.
Ijumaa saa tano kamili tulikusanyika kweny ukumbi wa chakula kwa lengo la kusikiliza mawaidha ya walimu ma mkuu wa shule ili shule ifungwe na kila mwanafunzi aelekee kwao kwa mapumziko ya kumaliza muhula wa masomo. Mkuu wa shule alisimama baada ya kukaribishwa na makamu wake tayari kwa kutufungia shule. Alianza kwa kusema, “Ndugu walimu wenzangu, wanafunzi na wafanyakazi wengine tofauti na walimu, awali ya yote sina budi kuwapa kongole zangu za dhati kwa kuliongoza jahazi la shule yetu mpaka hapa tunapokwenda kulifunga pazia la maosmo ya muula wa kwanza. Kila mmoja wetu ameweza kulitendea haki eneo lake la kazi ipasavyo pasina uvivu wowote. Kwa upande wa walimu wenzangu na wale msio walimu sikuweza kupokea taarifa zozote mbaya kutoka kwenu kupitia sanduku letu la maoni. Kwa hilo ninaomba muwapigie makofi wote.” Alipomaliza hayo aligeukia upande wa wanafunzi.
“Matatizo niliyokumbana nayo katika ofisi yangu kutoka kwa wanafunzi, yalikuwa ni mengi ambayo mengine yalihitaji kukaliwa na bodi ya shule ili kufanyiwa maamuzi anuai. Kumezuka tabia ambazo haziwezi kufumbiwa macho abadani. Sheria zetu za shule hasa ile ya namba saba, nane na tisa zinawakataza wanafunzi kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi , uvutaji na utumiaji wa madawa ya kulevya na utoro wa kutohudhuria vipindi darasani. Matendo hayo yamekuwa ni baadhi ya kero zilizonifikia ofisini kwangu kwa wingi. Na mimi bila hiyana niliyaundia tume mambo hayo ili yafanyiwe uchunguzi na jopo la walimu wangu ili haki itolewe. Mambo yaliyogundulika katika uchunguzi huo ni pamoja na mapenzi ya jinsia moja yanayofanywa na vijana wababe wa vidato vya juu kwa wenzao hawa wa vidato vya chini. Kilichogundulika kwa ushahidi wa picha zetu za mnato ni kwamba, vijana wengi walilazimishwa kufanyiwa kitendo hicho pasina ridhaa yao na wengine kwao ndio mchezo waliouzoea kwani wachunguzi wetu wameweza kubaini marudiano ya kitendo hicho kwa kugeuzana wanaume kwa wanaume.” Alipofikia maeneo hayo mkuu wa shule aliomba aletewe maji ya kipoza koo kisha akaendelea. “Wanangu wapendwa, kwa mujibu wa kitabu kitakatifu kijulikanacho kama Biblia, Mwenyezi Mungu aliweza kuziwasha moto Sodoma na Gomora kwa dhambi kama hiyo ya ushoga, hivyo basi, na mimi siwezi kulifumbia macho suala hilo. Kwa kuwa sikukabidhiwa moto au kibiriti, mimi nitazisimamia sheria na kanuni za shule kuwaondoa wale wote waliofumaniwa na mkasa huo uliofanyiwa uchunguzi mujarabu.”
Mkuu wa shule alihitimisha hotuba yake kwa kutujuza kwamba tarehe ya kufungua shule itaandikwa kwenye ripoti ya mwanafunzi ambapo kutakuwa na taarifa zote bila kuwasahau waliofukuzwa shule na waliopata msimamisho wa muda. Tulitawanyika kwa kila mtu kuangalia ustaarabu wa safari za kuelekea makwao.
Nikiwa bado najiandaa ili siku hiyo isinikute hapo shuleni, nilipokea taarifa kuwa madam Linda ana maongezi nyeti na mimi ya kunitakia likizo njema kama mtumiaji alivyonijuza. Awali nilitaka kuupuzia wito huo lakini moyo ulinisukumu kuufuata ili anipe umbeya wa ofisini isije kuwa na mimi ni miongoni mwa wanafunzi ambao wamekumbwa na msala huo. Niliacha kupanga mizigo yangu ili nikamsikilize madam na ujumbe wake ambao sikujua ulihusu nini. Nilibaki nikiwatazama baadhi ya wanafunzi wenzangu wakiliparamia basi la ‘Super Star’ na mimi nikielekea kwa madam kwa unyonge.
********
********
********
********
********
********
********
====>>Itaendelea Jumatatu...
Usiikose SEHEMU YA 24>>> ya Riwaya hii ifikapo siku ya Jumatatu wiki ijayo, na utaipata hapa Zero Degree pekee.
Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 23
Reviewed by Zero Degree
on
8/18/2017 07:09:00 PM
Rating: