Loading...

Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 24


MTUNZI: MC Short Charles Gwimo

Ilipoishia.........Nikiwa bado najiandaa ili siku hiyo isinikute hapo shuleni, nilipokea taarifa kuwa madam Linda ana maongezi nyeti na mimi ya kunitakia likizo njema kama mtumiaji alivyonijuza. Awali nilitaka kuupuzia wito huo lakini moyo ulinisukumu kuufuata ili anipe umbeya wa ofisini isije kuwa na mimi ni miongoni mwa wanafunzi ambao wamekumbwa na msala huo. Niliacha kupanga mizigo yangu ili nikamsikilize madam na ujumbe wake ambao sikujua ulihusu nini. Nilibaki nikiwatazama baadhi ya wanafunzi wenzangu wakiliparamia basi la ‘Super Star’ na mimi nikielekea kwa madam kwa unyonge.

Endelea nayo: Moyoni nilikuwa na simanzi kuu iliyosababishwa na kukatishwa kwa safari yangu ya kuelekea nyumbani huku nikiwazia kile nilichoitiwa na madam Linda ilihali shule imeshafungwa. Nilitembea kwa mwendo wa mzee Kobe huku nikiwashuhudia wenzangu wakiuparamia mlango wa basi kwa mashindano ya kuwahia siti za kukaa. Nilitembea bila uangalifu jambo ambalo lilinifanya nitipoteze uelekeo hadi nikajibamiza kichwa kwenye nguzo ya chuma iliyokuwa imesimikwa mkabala na ofisi ya mkuu wa shule. Kujibamiza huko kwa ghafla kichwani kulinitia maumivu makali mpaka nikapata maruweruwe ya kuziona nyota ilihali ni mchana.

*******

Baada ya kujigonga kwenye nguzo hiyo nilisimama kwa muda maeneo yale ili akili iweze kupambanua vizuri kati ya harufu ya kwapa na ile ya mwaranda. Akili ilipoweza kukaa sawa niliachana na fikra za safari na kuandamana na mawazo mapya ya kuwazia kile nilichoitiwa na madam. Nilipofika ofisini kwake nilimwamkia kwa heshima yetu ya siku zote, yaani Shikamoo lakini sikujibiwa hiyo salamu yangu. Madam alisimama kutoka kwenye kiti chake na kuja kunilaki mithili ya mtoto anavyompokea mzazi wake baada ya kutoonana kwa muda mrefu. Kwa kulijua hilo na mimi sikumfanyia ajizi kwani niliachia mikono yangu kishupavu kumpokea kwenye kifua changu kilichogawanyika sehemu kuu mbili kwa ujazo wa kimazoezi tofauti na vile vifua mjazo vya ubonge nyanya. Madam alining’ang’ania kama vile kamkamta mhalifu au mdeni sugu aliyewahi kumkimbia baada ya kumpa uroda na kukosa malipo. Mgandmano huo uliambatana na mabusu mfululizo kila eneo la kichwa changu hasa hasa masikioni na kwenye midomo yangu yaani “lips”.


*******

Nilijitoa kifuani kwa madam kisha nikayaweka makalio kwenye kiti cha wageni mle mle ofisini. Madam naye alikaa kwenye kiti chake kisha mazungumzo yetu yakaanza. “David kipenzi cha moyo wangu, nimekuita ofisini kwangu kwa lengo moja tu na wala sio vinginevyo. Nafahamu wazi umepakumbuka sana nyumbani kwenu, lakini unachotakiwa kukijua ni hiki, mwanaume siku zote hatakiwi kuwa na kiherehere cha kuwa na kumbukumbu za kupakumbuka nyumbani kwao haraka kiivyo. Ninachotaka kukuambia ni kwamba, leo hutaondoka na wenzako kuelekea likizo bali wewe utajiondokea siku ya Jumapili ili niweze kuwa na wewe kwenye kuliwazana na kukujulisha yaliyowakumba wenzako baada ya bodi ya shule kukaa. Ningekueleza mengi kwa muda huu lakini mengi nitakueleza tutakapofika ninapoishi.”


*******

Muda wote huo, madam alipokuwa ananielezea, hakusita kutumia miguu yake kunikanyagakanyaga kichokozi kupitia chini ya meza. Kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa mdhamini wangu wa masuala ya ‘pocket money’ hapo shuleni sikumuwekea pingamizi lolote juu ya hilo kwani niliyapokea maombi yake kwa moyo mkunjufu huku nikiongozwa na ule msemo wa lugha ya Kiswahili usemao, “Ukila na kipofu usimguse mkono.” Sikuwa na hofu yoyote kuelekea nyumbani kwake alipokuwa amepanga nyumba ya vyumba viwili na sebule. Kwani wanafunzi wengi na hata walimu walikuwa wakijua kuwa Madam Linda kwangu ni nasaba moja kumbe ni mtu na mpenzi wake tena waliofikia kwenye hatua ambayo haipimiki kwa macho ya nje. Nyumbani kwa madam pia sikuwa na hofu kwani hata wapangaji wenzake walikuwa wananitambua kama mmoja wa wanandugu halali kumbe nilikuwa mla ndani kwa ndani niliyesilimishwa kwa undugu feki.


*******

Nilirudi bwenini kuchukua mizigo yangu tayari kwa safari ya kuelekea masikani kwa madam maeneo ya mji mwema. Tulipanda vipanga vya kutoka katonga kwenda mwanga maweni kisha tukashukia maeneo ya bima. Kwa kuwa kituo hakikuwa mbali na nyumba ilipo, tulitafuta wabeba mizigo wa kutumia toroli kisha tukawalipa. Kwa kuwa sikuwa mgeni wa maeneo hayo kama nilivyokujuza hapo awali nilichanganya fito zangu hadi masikani huku nikimuacha madam akija kwa miondoko ya kike kike. Nilipokelewa kwa furaha sana na wapangaji wengine ambao tulifahamiana kwa mara ya kwanza tulipoomba hifadhi ya mapumziko ya pasaka na madam kunitambulisha kama mdogo wake kamili niliyeambatana na marafiki zangu. Miongoni mwa madada walionipokea kwa mashamsham zaidi alijulikana kwa jina la Zabibu na kwa watoto wazuri ambao huwa ninajiaminisha kuwa waliumbwa kabla muumbaji hajachoka nahisi hata Zabibu alikuwemo. Naomba nisikupe wasifu wake kwa kina nikamsahau madam na pale nilipomuacha.


*******

Nilitulia sebuleni kwa mwenyeji wangu kwa mtindo wa kujilaza sofani kama mtu aliyechoshwa kwa safari ndefu. Hatimaye madam aliwasili tukaungana pamoja pale sebuleni. Kwa kuwa tulikuwa na njaa, madam hakupoteza muda mwingi pale sebuleni bali alibadilisha nguo kisha akaelekea jikoni kutayarisha maakuli. Akiwa kwenye maandalizi ya chakula hakuwa mzito sana kwani aliweza kuniandalia hata maji ya kuoga kisha nikaelekea bafuni kuoga. Kwa kuwa bafu lilikuwa la nje na upande huo wa nje ulitawaliwa na wapangaji tofauti tofauti wengi wao wakiwa wasimbe kama kina Zabibu, niliona soni kukatiza mbele ya wasimbe hao na bukta hivyo niliona ni vema nikautendea haki mwili wangu kwa kuvalia ‘traksuti’ yangu ya mazoezi.


*******

Niliingia bafuni ili nifanye usafi wa mwili wangu ambao haukupata maji ya kutosha kutokana na kukatika kwa maji pale shuleni na msongamano wa mitihani. Nilitumia muda mwingi kuufanyia usafi wa kina mwili wangu ili niupunguze uzito uliotokana na kutopata maji vizuri kwa takribani muda wa wiki mbili. Nikiwa katikati ya safari yangu ya kuoga, nilishtushwa na mchakato kama vile mpapaso wa mikono ya mtu ikielekea kwenye vitundu vya madirisha ya bafu yaliyokuwa upande wangu wa kushoto. Nilijifuta mapuvo usoni kwa haraka ili nimtazame huyo anayeendeleza unyambilisi huo ni nani. Hakika sikuamini macho yangu kama kile ninachokiona ni halisi. Kwa hamaki nilikumbana na uso mweupe wa Zabibu ukijaribu kupiga chabo bafuni kwa lengo la kuchukua sinema ya bure kuhusiana na maumbile yangu. Pale tulipokutanisha macho na Zabibu, alipata mshtuko wa ghafla kitendo kilichomfanya adondoke chini puuuu! Kama vile furushi la mitumba lililoporomoka kutoka garini.


*******

Nilijichekea moyoni huku nikijiuliza maswali yasiyo na majibu kamili kuhusu kupigwa chabo na Zabibu. Niliwaza hata yale yasiyowazika kwani nilihisi kuwa Zabibu alinifahamu fika kuwa mimi na jando au tohara tuna uadui wa muda mrefu. Hili nililihisi kwani ilishawahi kunitokea kwa Zabibu kutaka nioge naye nilipokuja hapo kwa madam kwa mara ya kwanza msimu ule wa likizo ya pasaka. Kilichoniumiza roho zaidi ni yale maneno aliyowahi kuniambia wakati ule “Kijana mzuri namna hiyo hautaki kuoga na vimwana kama sisi au una zunga nini?”………….… ukweli ulibakia huo huo mpaka muda huo nakanyaga tena mahali hapo kwa mara ya pili. Kitendo cha kutofanyiwa tohara kilinifedhehesha sana kwani hakikuweza kunipa uhuru wa kufanya mambo mubashara kama wengine wafanyavyo.

====>>Itaendelea Jumatatu...

Usiikose SEHEMU YA 25>>> ya Riwaya hii ifikapo siku ya Jumatatu wiki ijayo, na utaipata hapa Zero Degree pekee.
Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 24 Fumanizi la Mapenzi: Sehemu ya 24 Reviewed by Zero Degree on 8/25/2017 03:27:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.