Loading...

Kampuni ya SportPesa sasa yatua Afrika Kusini, yadhamini klabu ya Cape Town City


KLABU ya Cape Town City inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini maarufu kama PSL, imekuwa klabu ya kwanza kutoka nchini humo kudhaminiwa na Kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa.

Klabu hiyo ambayo ilimaliza nafasi ya tatu ya kwenye msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini msimu uliopita wa 2016/17 imeingia makubaliano ya udhamini huo kwa mkataba wa rekodi wa miaka minne na SportPesa ambao ndio watakuwa wadhamini wao wakuu kwenye jezi zao pamoja na kuwa washirika rasmi wa klabu hiyo katika michezo ya kubashiri. 

Mkurugenzi wa SportPesa Afrika Kusini, Nick Ferguson pamoja na Mmiliki wa klabu ya Cape Town, John Comitis walisaini makubaliano hayo jijini Cape Town jana Ijumaa huku magwiji hao wa michezo ya kubashiri duniani wakitambulisha uwepo wao kwenye Ligi hiyo ambayo inatajwa kuwa ligi tajiri zaidi barani Afrika.

“Tunawakaribisha washirika wetu wa kwanza nchini Afrika Kusini ambao ni Cape Town City FC kwenye familia yetu ya SportPesa. Udhamini huu ni uthibitisho kutoka SportPesa kuwa tumejidhatiti katika kuhakikisha tunachangia maendeleo ya mpira wa miguu kwenye nchi hii. 

“Tuna furaha kubwa sana kufanya kazi na Cape Town City FC, klabu ambayo inaendana na thamani yetu na tunatazamia kuwa na kipindi cha mafanikio ambacho kitahamasishwa na safari hii ambayo tumeianza pamoja”, alisema Ferguson wakati wa sherehe ya kutiliana saini. 

Nembo ya SportPesa sasa itakuwa ikionekana upande wa mbele wa jezi rasmi ya Cape Town City FC baada ya timu hiyo kuingia kwenye orodha ya timu kubwa za mpira wa miguu duniani zinazodhaminiwa na kampuni hiyo.

Makubaliano haya yanahusisha timu ya wakubwa, timu B na timu za vijana za Cape Town City, ambayo itashiriki kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika kwa mwaka 2018 baada ya kumaliza nyuma Bidvest Wits na Mamelodi Sundowns katika msimamo wa Ligi ya Afrika Kusini

Klabu hiyo ilianzishwa na mfanyabiashara John Comitis ambaye ni mmiliki wa zamani wa Cape Town Spurs na mwanzilishi wa Ajax Cape Town mwaka 2016 ambapo ndipo Cape Town City FC ilizaliwa upya ikiwa ni miongoni mwa klabu zilizotamba nchini Afrika Kusini katika miaka ya 1960 na 1970.

Simba, Yanga na Singida United ni miongoni mwa klabu zinazodhaminiwa na SportPesa kwa hapa nchini huku kwa upande wa England Everton nayo ikiwa mojawapo.
Kampuni ya SportPesa sasa yatua Afrika Kusini, yadhamini klabu ya Cape Town City Kampuni ya SportPesa sasa yatua Afrika Kusini, yadhamini klabu ya Cape Town City Reviewed by Zero Degree on 8/12/2017 10:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.