Loading...

Wabunge waikomalia Idara ya Uhamiaji


Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac) imeibana Idara ya Uhamiaji baada ya kubaini upungufu katika taarifa zake za fedha, utoaji wa viza kugubikwa na mazingira ya rushwa na upotevu wa mapato.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Munde Tambwe amesema leo Agosti 30 kuwa Idara ya Uhamiaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baadhi ya watumishi wake wamegubikwa na mazingira ya rushwa.

Ametoa mfano wa wawekezaji kutoka China ambao walifika nchini kuingia makubaliano ya kuwekeza katika kiwanda cha kusindika tumbaku mkoani Tabora lakini waliondoka baada ya kukosa viza kwa kuwekewa mazingira ya rushwa.

Munde ametoa mfano mwingine wa wageni wa mmoja wa wadau wa Klabu ya Simba waliofika nchini wakitokea Ivory Coast ambao walitaka viza ya kwenda Vietnam.

Amesema Idara ya Uhamiaji iliwanyima viza hiyo na kuwataka warejee kwao ambako wataipata.

“Inatia aibu mwenyekiti wanatengeneza mazingira ya rushwa tu. Mtu akitaka viza pale Airport (uwanja wa ndege) anakaa saa mbili tofauti na nchi zingine duniani viza huchukua dakika 45 hadi saa moja,” amesema. 

Mbunge wa Magomeni (CCM), Jamal Kassim amesema ofisi ya CAG ilifanya utafiti Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kubaini kati ya wageni 65 walioingia nchini, 20 hawakuwa na taarifa za viza.

“Udhibiti na ulipaji wa viza ni dhaifu hali inayosababisha mapato ya Serikali kupotea,” amesema. 

Akizungumzia madai hayo, Kamishna wa Fedha na Utawala wa Uhamiaji, Edward Chogero amesema viza ni changamoto nchini.

Mwenyekiti wa kikao hicho, Japhet Hasunga ambaye ni mbunge wa Vwawa amesema kamati inamwagiza ofisa masuhuli (Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya

Ndani ya Nchi) kuimarisha mfumo wa udhibiti kuzuia upotevu wa fedha katika mapato yanayotokana na viza.
Wabunge waikomalia Idara ya Uhamiaji Wabunge waikomalia Idara ya Uhamiaji Reviewed by Zero Degree on 8/30/2017 11:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.