Loading...

Wenyeviti wa vijiji matatani kisa kupokea rushwa


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara, imewafikisha mahakamani Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyanduga, Wilaya ya Rorya, Andele Sion’go (47) na mwananchi aitwaye Monica Mayala (25) kwa tuhuma za kupokea rushwa.

Washtakiwa walifikishwa mahakamani Jumatatu mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Tarime, Martha Mpaze na kusomewa shtaka lao na Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Mwinyi Yahaya.

Upande wa mashtaka ulidai Agosti 10, mwaka huu, Sion’go na Mayala walipokea rushwa ya Sh. 180,000 kutoka kwa Bahati Odingo kama kishawishi cha kutokwenda kutoa ushahidi dhidi yake katika kesi ya jinai iliyofunguliwa mahakama ya mwanzo Tarime.

Katika tukio lingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ryagoro, James Risso (61), Jumatatu alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Amon Kahimba, akituhumiwa kupokea rushwa.

Yahaya alidai Agosti 11, mwaka huu, majira ya saa tano asubuhi, kwenye ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Ryagoro, mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh. 50,000 kutoka kwa Kevin Wadugu ili ampatie mlalamikaji nakala ya hukumu na mwenendo wa shauri la ardhi lililopo katika Baraza la Ardhi ya Serikali ya Kijiji.

Washtakiwa walifikishwa mahakamani wakituhumiwa kutenda makosa hayo kinyume cha kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Takukuru namba 11 ya mwaka 2007.

Walikana mashtaka dhidi yao na walipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambapo kila mmoja alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye kadi za kupigia kura na barua za utambulisho na kila mdhamini kusaini bondi ya Sh. milioni mbili.

Kesi zote mbili ziliahirishwa hadi Agosti 29, mwaka huu zitakapotajwa kwa kuwa uchunguzi wa kesi ya kwanza haujakamilika na ya pili itapangiwa tarehe ya usikilizaji wa hoja za awali.
Wenyeviti wa vijiji matatani kisa kupokea rushwa Wenyeviti wa vijiji matatani kisa kupokea rushwa Reviewed by Zero Degree on 8/19/2017 01:57:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.