Loading...

Polisi yatoa ufafanuzi kuhusu watoto waliokufa baada ya kulipukiwa na bomu Arusha


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha Bw.Charles Mkumbo amewataka viongozi katika maeneo yaliyoko karibu na kambi za mazoezi ya kijeshi kuweka utaratibu wa kuwakumbusha wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona vitu wasivyovijua hasa vyenye asili ya chuma ili kuepusha madhara yasiyo ya lazima.

Kamanda Mkumbo ametoa hadhari hiyo alipokuwa akizungumzia tukio la vifo vya watoto watatu wakazi wa kata ya Lokisale wilayani Monduli vilivyosababishwa na mlipuko wa bomu waliookota wakati wanachunga mifugo na kuanza kulichezea kama mpira ambalo lililipuka na kuwajeruhi vibaya miguuni.

Akizungumza kwa njia ya simu kamanda Mkumbo amesema licha ya kuwa tukio hilo ni la bahati mbaya lakini lingeweza kuepukika kama watoto hao wangeweza kuepuka na kutoa taarifa ya kitu walichokiona suala ambalo pia wangeweza kufanya hivyo kama wangekuwa wanakumbushwa na wazazi wao mara kwa mara wanapokwenda machungani.

Akizungumza pia kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya Monduli Bw. Iddy Kimanta amesema watoto hao wote ni wanafunzi wa shule ya msingi Nafuko na wawili akiwemo Landisi Setabau miaka 12 na Samweli Nyandusi miaka 9 walikuwa wanasoma darasa la kwanza wakati mwingine aliyetajwa kwa jina la Seuri Losila miaka 9 alikuwa darasa la tatu.

Viongozi wa eneo lililopotokea tukio hilo wamesema kimsingi tukio hilo ni bahati mbaya kwani kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakielimishwa na wanaelewa na pia kufuata maelekezo na mara nyingi wamekuwa wakishitoa ushirikiano ukiwemo wa kutoa taarifa wanapoona mabaki ya vyuma na kwamba kimsingi ni tukio la bahati mbaya.

Kwa mujibu wa viongozi hao katika maeneo mengi ya wafugaji wakati wa likizo watoto huwasaidia wazazi wao kuchunga mifugo na pia wakati wote wamekuwa wakitoa taarifa wanapokutana na vitu kama hivyo na wahusika wamekuwa wakifika mara moja na kuvichukua.

Source: ITV
Polisi yatoa ufafanuzi kuhusu watoto waliokufa baada ya kulipukiwa na bomu Arusha Polisi yatoa ufafanuzi kuhusu watoto waliokufa baada ya kulipukiwa na bomu Arusha Reviewed by Zero Degree on 9/18/2017 04:42:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.