Loading...

Tiketi za Kombe la Dunia 2018 zaanza kuuzwa

Kundi la kwanza la tiketi za fainali za Kombe la Dunia 2018 ambazo zitachezewa nchini Urusi zilianza kuuzwa Alhamisi.

Mashabiki wa soka wanaweza kuwasilisha maombi ya kununua tiketi hizo kupitia tovuti ya Fifa.

Tiketi hizo zitauzwa kwa awamu mbili.



Bei ya tiketi hizo itakuwa ni kuanzia paundi 79 kwa mechi za raundi ya pili hatua ya makundi hadi paundi 829 kwa fainali yenyewe ambayo itachezewa Moscow.

Kwa kufuata sera za awali za uuzaji wa tiketi, wakazi wa urusi watakuwa na aina maalum za tiketi ambazo bei yake itaanzia paundi 17.

Tiketi ghali zaidi zitakuwa za mechi ya fainali yenyewe ambazo zitauzwa paundi 829.

Hilo litakuwa ni ongezeko la paundi 151 ukilinganisha na tiketi za mechi sawa za fainali ya mwaka 2014 ambayo ilichezewa Rio de Janeiro nchini Brazil.


"Tumeweka mfumo wa kutoa tiketi ambao utawapa mashabiki nafasi sawa ya kujipatia tiketi," katibu mkuu wa Fifa Fatma Samoura amesema.

Awamu ya kwanza ya kuwasilisha maombi ya tiketi itafanyika kabla ya tarehe 12, mwezi Oktoba.

Watakaowasilisha maombi watafahamishwa kufikia 16 Novemba iwapo wamefanikiwa.

Michuano hiyo itaanza tarehe 14 Juni ambapo Urusi watacheza mechi ya ufunguzi uwanjani Luzhniki, Moscow.

Mataifa saba tayari yamejikatia tiketi ya kushiriki michuano hiyo pamoja na mwenyeji Urusi - mabingwa mara tano Brazil, Ubelgiji, Iran, Mexico, Japan, Saudi Arabia na Korea Kusini.
Tiketi za Kombe la Dunia 2018 zaanza kuuzwa Tiketi za Kombe la Dunia 2018 zaanza kuuzwa Reviewed by Zero Degree on 9/16/2017 11:03:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.