Loading...

Watano wakamatwa na polisi kwenye doria ya kuzuia maombezi ya Tundu Lissu

Watu watano wanaosadikika kuwa ni wanachama wa CHADEMA wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa mahojiano zaidi kujua kama walikuwa na mpango wa maombezi ya Mhe. Tundu Lissu uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Tip -Sinza, wilayani Ubungo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Murilo Jumanne aliyekuwa uwanjani hapo na kikosi cha askari wapatao 25 amesema watu hao walikamatwa saa 3 asubuhi wakiwa katika eneo hilo.

“Tunawashikilia na tutawahoji kama wana uhusiano na kile kilichopangwa kufanyika hapa kwa sababu kilishapigwa marufuku. Kama hawana uhusiano tutawaachia,” amesema Kamanda Jumanne kwenye mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi huku akiwaonya Wananchi waliopanga kufanya maombi hayo.

“Atakayetaka kujaribu aje ila cha moto atakiona kwa sababu jitihada za kuzuia watu wema wasikanyage hapa zimeshafanyika sasa wanakuja kufuata nini.”

Baadhi ya polisi wameonekana wakiwa na mabomu ya kutoa machozi na walifika uwanjani hapo wakiwa kwenye magari aina ya Toyota Land Cruiser.

Doria hiyo inakuja baada ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) jana Jumamosi kutoa taarifa kuwa leo litaungana na viongozi wa kiroho kufanya maombi maalumu kumwombea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu anayeendelea na matibabu Nairobi, nchini Kenya baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7.
Watano wakamatwa na polisi kwenye doria ya kuzuia maombezi ya Tundu Lissu Watano wakamatwa na polisi kwenye doria ya kuzuia maombezi ya Tundu Lissu Reviewed by Zero Degree on 9/18/2017 08:00:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.