Loading...

Zitto Kabwe amtega Rais Magufuli


Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe amesema kuwa atakuwa tayari kuwajibika endapo Rais Dkt John Magufuli ataruhusu uchunguzi huru wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mapato ya serikali yatakutwa hayajashuka kama ambavyo amekuwa akisema.

Zitto ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja tangu Rais Magufuli alipokanusha madai yake akivitaka vyombo vya dola kuwafikisha mahakamani watu wanaobadilisha takwimu za serikali wakiwamo wanaosema kuwa mapato ya serikali yameshuka wakati sio kweli ili wakathibitishe kauli yao.

“Kama Rais anaamini kuwa Mapato hayajaporomoka, aruhusu ukaguzi maalumu wa CAG kwenye Mapato ya July na Agosti 2017 na ukaguzi huo uwekwe wazi Kwa umma. Rais akifanya hivyo NITAWAJIBIKA.”

Katika taarifa yake, Zitto amezidi kusimamia msimamo wake akidai kuwa taarifa za mapato za hivi karibuni zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni za uongo, na kwamba, taarifa ya kupikwa kwa takwimu za Pato la Taifa wataitoa mara baada ya kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Act Wazalendo kitakachoketi 28/10/2017.

Aidha, ameeleza kuwa, Sheria ambayo Rais aliviagiza vyombo vya dola kuitumia ili kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wanaopotosha takwimu za serikali, haizuii tafsiri za takwimu zinazotolewa na Serikali.

“Tunatumia takwimu za Serikali kuonyesha kuwa Serikali inadanganya Kwa kutokusema ukweli wote wa uhalisia wa uchumi na kuporomoka Kwa mapato.”

Zitto amekanusha taarifa ya Rais kuwa mapato ya serikali yameongezeka ndio sababu wanaweza kutekeleza miradi mikubwa, akisema kuwa serikali imekuwa ikikopa bila kutoa taarifa pamoja na kutumia fedha za taasisi za serikali kinyume na sheria ambapo pia ni kinyume na katiba ya nchi.

“Rais anajua kuwa Serikali inatumia, bila kufuata sheria, Fedha za Mashirika ya Umma zilizopo Benki Kuu kulipia baadhi ya Miradi yake. Kukiuka sheria za Fedha ni kosa la jinai na wakati mwengine kosa la kikatiba kwani Katiba imeweka utaratibu wa masuala ya Fedha za Umma,” ameandika Zitto.

“Kodi inayokusanywa na TRA inaweza kulipa mishahara na kuhudumia Deni la Taifa tu. Kwanini Rais wetu hasemi kuwa tunakopa? Kukopa sio dhambi, kwanini aaminishe watu kuwa anatekeleza miradi Kwa kuwa kodi zimeongezeka,?” alihitimisha Zitto.
Zitto Kabwe amtega Rais Magufuli Zitto Kabwe amtega Rais Magufuli Reviewed by Zero Degree on 10/25/2017 09:53:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.