Loading...

17 waokolewa, wawili wasadikika kufa kwa ajali ya Boti Ziwa Victoria


Watu 17 wameokolewa na wengine wawili wakisadikika kufa maji baada ya boti ya mizigo ya MV Julius kuzama ziwa Victoria jana usiku ikiwa na watu pamoja na mizigo, wakitoka kisiwa cha Goziba Wilayani Muleba Mkoani Kagera.

Inasemakena boti hiyo inayofanya shughuli zake za usafirishaji kati ya Mwanza na kisiwa cha Gozba Wilayani Muleba Mkoani Kagera, ilizama majira ya saa nne usiku ikiwa na nahodha, wabeba mizigo pamoja na mzigo wa magunia 750 ya dagaa.

Diwani wa Kata ya Goziba, Masaba Nkunami amesema boti hiyo imezama usiku wa kuamkia leo Alhamisi muda mfupi baada ya kuanza safari zake kutoka kisiwani hapo.

Licha ya kutotaja idadi kamili ya watu waliokuwamo kwenye boti hiyo ya mizigo, Nkunami amesema kwa sasa wanaendelea na jitihada za kuwatafuta watu wawili wanaosadikika kuzama ziwani. 


Amesema boti hiyo iliundwa kwa vyuma mfano wa meli ambayo hufanya shughuli za kusafirisha mizigo kati ya kisiwa cha Goziba na Mwanza.

“Jitihada za kutafuta watu hao zinaendelea hadi sasa watu wapo majini wakiwatafuta, hivyo taarifa zaidi zitatolewa baadaye,” amesema Nkunami.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi amekiri kuzama kwa boti hiyo lakini akasema “mpaka sasa hakuna taarifa za vifo.”

Jeshi la Polisi linaendelea kufuatilia kubaini kama kuna waliosahaulika majini, na taarifa zaidi zitatolewa baada ya zoezi hilo kukamilika.
17 waokolewa, wawili wasadikika kufa kwa ajali ya Boti Ziwa Victoria 17 waokolewa, wawili wasadikika kufa kwa ajali ya Boti Ziwa Victoria Reviewed by Zero Degree on 11/16/2017 07:21:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.