Loading...

Faida za Vitunguu Swaumu kwenye masuala ya Urembo


IMEELEZWA kuwa licha ya vitunguu swaumu kuwa miongoni viungo muhimu kwa chakula, imebainika kuwa zao hilo lina faida nyingi kwa walaji ikiwamo kusaidia mwili kukabiliana na maradhi mbalimbali na pia huwaongezea urembo kina dada.

Rejea mbalimbali za masuala ya lishe na afya zinaonyesha kuwa vitunguu swaumu ni miongoni mwa jamii ya vyakula vyenye kutibu baadhi ya magonjwa na pia huukinga mwili dhidi ya mashambulizi ya maradhi pindi vikitumika vyema.

Aidha, imefahamika kuwa kwa sababu ya nguvu yake ya kuua vimelea vya magonjwa, hivi sasa vitunguu swaumu hutumika kama malighafi ya kutengenezea baadhi ya dawa za binadamu.

Taarifa iliyotolewa na gazeti maarufu humu nchini inadai Dkt. Abdallah Mwindah wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), alisema vitunguu swaumu ni tiba kwa sababu vina viinilishe vyenye uwezo wa kuondoa sumu mbalimbali mwilini. 


Alisema vitunguu swaumu husaidia kuondoa mabaka, harara kwenye ngozi na kudhibiti mba kichwani. Imebainika kuwa kwa sifa hizo, kina dada wenye kupenda masuala ya urembo ni muhimu kwao kwa sababu huimarisha afya ya ngozi zao na kuziongezea mwonekano wa kuvutia.

Akieleza zaidi, Dk. Mwindah alisema vitunguu swaumu husaidia kusafisha njia ya mkojo na hivyo kuusaidia mwili kukabiliaana na maradhi ya U.T.I, huvunjavunja mawe katika figo na pia huupa nguvu ubongo wa mlaji wa zao hilo.

“Kitunguu swaumu kinasafisha tumbo, huwatibu wale wenye matatizo ya kuhara damu, huyeyusha mafuta mabaya mwilini, hutibu ugonjwa wa matumbo wa amoeba, bakteria na minyoo,” alisema. 

Faida nyingine za vitunguu swaumu, kwa mujibu wa Dk. Mwindah, ni kuondoa gesi tumboni na pia husaidia kutibu ugonjwa wa homa ya matumbo (typhoid).

“Husaidia kutibu magonjwa ya kikohozi unapokula kitunguu, pia wale wanaosumbuliwa na meno ulaji wa kitunguu swaumu husaidia kuzuia meno kung’oka na hutuliza maumivu ya meno,” alisema. 

Alitaja faida nyingine kuwa ni husaidia kuongeza nguvu za kiume, hutibu maumivu ya kichwa, kizunguzungu, shinikizo la damu, kisukari na pia kudhibiti baadhi ya saratani.

Faida nyingine kati ya nyingi za vitunguu swaumu mwilini, kwa mujibu wa Dk. Mwendah, ni kusaidia kuongeza nguvu kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, kuzuia damu kuganda, kutibu ukosefu wa usingizi, kuleta hamu ya kula na huongeza kinga ya mwili na pia husaidia kuondoa mafuta kwenye mishipa ya damu.

Kadhalika, alisema vitunguu swaumu vina manganese inayosaidia kutengeza mifupa, vina vitamini B6 inayosaidia ufanyaji kazi wa ubongo na mishipa na pia husaidia kuweka sawa mfumo wa sukari mwilini.

JINSI YA KUTUMIA:

Baadhi ya wataalamu wa lishe wanashauri kuwa mlaji anaweza kutumia vitunguu swaumu kwa kumeza punje zake kama dawa.

Kwa kupikia kwenye vyakula, menya maganda yake kwa kiwango cha mahitaji ya mboga na kisha twanga, hakikisha vimelainika na baada ya hapo vyaweza kuwekwa kwenye mboga au kwa mapishi ya pilau.

Inaelezwa kuwa pia unaweza kuviweka kwenye mchanganyiko wa matunda, kusaga mchanganyiko na kuunywa.
Faida za Vitunguu Swaumu kwenye masuala ya Urembo Faida za Vitunguu Swaumu kwenye masuala ya Urembo Reviewed by Zero Degree on 11/12/2017 04:27:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.