Loading...

Katekista afariki muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza ibada ya mazishi


MWALIMU wa dini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mpanda, Noel Sitemele amefariki dunia muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza ibada ya mazishi ya muumini wake yaliyofanyika katika makaburi ya Mchakamchaka Kijiji cha Majalila wilayani Tanganyika mkoani Katavi.

Katekista huyo alikuwa akitoa huduma ya kiroho katika Kigango cha Mchakamchaka kilichopo katika Parokia ya Mpanda Ndogo katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi. Akizungumzia mkasa huyo, Diwani wa Kata ya Mpanda Ndogo, Hamad Mapengo alisema licha ya Sitemele kuwa mwalimu wa dini, katika uhai wake alikuwa pia Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila kilichopo katika Halmashauri ya Mpanda wilayani Tanganyika.
Diwani wa Kata ya Mpanda Ndogo, Hamad Mapengo (Picha ya mtandao)
Mapengo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpanda, alisema Katekista alifariki dunia juzi saa 11 jioni muda mfupi baada ya kufikishwa zahanati ya kijijini Majalila kutibiwa. Alisema kabla ya kukutwa na umauti, Katekista huyo alikuwa mwenye siha njema na aliongoza ibada ya mazishi ya muumini wake hadi mwisho katika makaburi ya Kigango cha Mchakamchaka kilichopo katika Kijiji cha Majalila ambapo alianza kujisikia vibaya.

“Baada ya kumaliza ibada hiyo ya mazishi, alianza kujisikia vibaya hivyo akalazimika kurejea nyumbani kwake na kuwaacha waombolezaji makaburini,” alieleza Mpaengo. Alisema, baada ya kufika nyumbani kwake, hali yake iliendelea kuwa mbaya na aliomba msaada kutoka kwa majirani zake wamkimbize kwenye kituo cha afya kwa matibabu.

Inaelezwa zahanati hiyo haiko mbali kutoka alikokuwa akiishi mwalimu huyo wa dini. Mwenyekiti alisema, taarifa za kifo cha Katekista huyo zilizagaa haraka kijijini humo na kuwafikia waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu aliyeongozewa ibada ya mazishi na Katekista huyo waliopata simanzi kubwa huku wengine wakiwa hawaamini jambo hilo.

Maziko yake yalifanyika jana katika makaburi ya kigango cha Mchakamchaka Kijiji cha Majalila na 
ibada ya mazishi ya katekista huyo yaliyohudhuriwa na mamia ya waombolezaji akiwemo Mbunge wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso iliongozwa na Padri Paschal Kipenye wa Parokia ya Mpanda Ndogo.

Source: Habari Leo
Katekista afariki muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza ibada ya mazishi Katekista afariki muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza ibada ya mazishi Reviewed by Zero Degree on 11/27/2017 06:35:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.