Loading...

Watakaoshindwa kudhibiti walimu watoro kuchukuliwa hatua

Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa ( TAMISEMI ), Tixon Nzunda
Wakurugenzi Watendaji na Maofisa Elimu wa Ngazi zote wameagizwa kuhakikisha wanawachukulia hatua walimu wote wenye tabia za utoro kwa sababu wamekuwa wakichangia kufanya vibaya kwa wanafunzi katika baadhi ya shule hapa nchini.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Tabora na Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais , Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa( TAMISEMI ), Tixon Nzunda wakati akizungumza na Watendaji na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Manispaa ya Tabora , Halmashauri za Wilaya ya Sikonge, Uyui , Kaliua na Urambo.

Alisema kuwa takwimu za kitafiti zinaonyesha kuwa asilimia 56 ya walimu wanatabia ya utoro na asilimia 44 ndio sio watoro na ndio wanaofanyakazi kwa bidii na kutoa matokeo mazuri.

Nzunda alisema kuwa utoro huo upo katika aina mbalimbali ambazo ni walimu kukosekana shuleni bila maelezo, wengine wanasaini vitabu vya mahudhurio lakini hawaingii madarasani kufundisha, wakati wapo wanaoingia makubaliano na walimu wakuu wa shule na kuhudhuria shule na kundi la mwisho ni wale wapo shule lakini hawafundishi.

Alisema kuwa hatasita kumckulia hatua kali ikiwemo kumuondoa Kiongozi katika nafasi yake atakayeshindwa kudhibiti utoro wa walimu kwa kuwa atakuwa hatoshi katika nafasi ya kuwa kiongozi.

Nzunda alisema kuwa hairusiwi Mwalimu kutoka katika Kituo chake cha kazi bila ruhusa ya mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na ikibainika Mwalimu ameondoka katika eneo lake la kazi bila idhini ya Afisa Masuhuli basi Mkuu wa Shule atawajibika na mhusika atachukulia hatua za kisheria.

Katika hatua nyingine Naibu Katibu Mkuu huyo aliwaagiza Wakuu wa Shule zote nchini kuhakikisha wanashirikiana na wazazi katika kudhibiti utoro wa wanafunzi ambao wamekuwa wakishindwa kuhudhuria shule na wengine kuishia katika bila kumaliza elimu yao ya msingi.

Alisema kuwa tafiti zinaonyesha kuwa katika asilimia mia ya watoto wanaoingia shule ni asilimia 70 tu ndio wanaomaliza Shule na 30 inaishia njiani.

Nzunda alisema kuwa hiyo asilimia 30 inaishia njiani ndio inayosababisha kuzalisha makundi mbalimbali yakiwemo ya uhalifu na watoto wa mitaani ambao baadae wanakuwa mzigo kwa Taifa.

Alisema kuwa kuanzia sasa ni vema walimu wakahakikisha wanafuatilia watoto wote walioandikishwa wawepo Shule na kama mzazi anasema amehamia kwingine wafuatile kujua ukweli ili kudhibiti udanganyifu unaolenga kumkatisha mtoto kwa ajili ya kumpeleka katika shughuli mbalimbali ikiwemo kumtumikisha na kumuozesha.

Naibu Katibu Mkuu yupo katika ziara ya kikazi katika Mikoa ya Kigoma, Tabora na Singida kwa lengo ya kuhimiza usimamizi bora wa sekta ya elimu , kilimo, mifugo , utawala bora na mengine mengi.
Watakaoshindwa kudhibiti walimu watoro kuchukuliwa hatua Watakaoshindwa kudhibiti walimu watoro kuchukuliwa hatua Reviewed by Zero Degree on 11/18/2017 08:37:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.