Loading...

Rais Magufuli asaini nyaraka za msamaha kwa wafungwa 63

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akitia saini Nyaraka zenye majina ya Wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa pamoja na majina mawili ya Familia ya Nguza Viking (Babu Seya), na Johnson Nguza waliopata msahama wa Rais, katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. Kulia ni Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma Malewa akishuhudia
Rais John Magufuli ametia saini nyaraka za msamaha alioutoa kwa wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na wawili Nguza Viking (Babu Seya) na Johnson Nguza (Papii Kocha) waliohukumiwa kifungo cha maisha jela.

Rais Magufuli ametia saini nyaraka hizo leo Jumapili Desemba 10,2017 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Msamaha huo aliutoa jana Jumamosi Desemba 9,2017 katika maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara).

Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri ya kurekebisha tabia za wafungwa.

Taarifa ya Ikulu imesema Rais Magufuli amesisitiza kuwa pamoja na kutolewa msamaha huo, vyombo vya dola viendelee kusimamia sheria.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiyahakiki kwa kuyasoma majina ya Wafungwa 63 waliopata msahama wa Rais kabla ya kutia saini Nyaraka hizo za Msamaha katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma. Kulia ni Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma Malewa akishuhudia
Amelitaka Jeshi la Magereza kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha mali, yakiwemo mazao ya kilimo na kufanya kazi za ujenzi.

“Nimeona nitumie kifungu hiki cha Katiba -Ibara ya 45 (1) ambacho nilipewa na Watanzania, ingawa kilikuwa hakijawahi kutumika, unajua mtu ambaye alihukumiwa kunyongwa halafu baadaye anaachiwa, ni kitu kinashangaza kwa sababu hakijawahi kutokea, lakini nimeona nifanye hivyo kwa ajili ya Watanzania,” amesema. 

Rais Magufuli amesema, “Muendelee kusimamia wajibu wenu na kusimamia sheria, mtu anayehukumiwa kufungwa afungwe kweli, na nilishatoa wito kwa magereza, pasiwepo wafungwa wa kukaa tu na kupumzika, wafanye kazi, kufungwa si kustarehe.” 

Akizungumzia hilo, Kamishna Jenerali wa Magereza Dk Juma Malewa amemshukuru Rais kwa kutoa msamaha huo wa kihistoria.

Amesema wafungwa na maofisa Magereza wameipongeza hatua hiyo ambayo itasaidia kuwatia moyo wafungwa wanaorekebishwa tabia katika magereza nchini.

Kamishna Jenerali Malewa amesema wafungwa waliopatiwa msamaha wa kuachiwa huru, waliruhusiwa kutoka magerezani tangu jana.

Amesema maofisa Magereza wamewaasa kwenda kuonyesha mfano bora kwenye jamii watakakokwenda kuishi.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza agizo lake la kutengeneza viatu kwa ajili ya askari badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini Dkt. Juma Malewa mara baada ya kutia saini majina ya wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa pamoja na majina mawili ya Wafungwa Nguza Viking(Babu Seya), na Johnson Nguza waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha maisha jela
Jeshi la Magereza linazalisha jozi 150 za viatu kwa siku katika kiwanda cha Karanga kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kwa kushirikiana na mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF, jeshi hilo limeanza kuboresha kiwanda hicho ili kufikia uzalishaji wa jozi 450 kwa siku.
Rais Magufuli asaini nyaraka za msamaha kwa wafungwa 63 Rais Magufuli asaini nyaraka za msamaha kwa wafungwa 63 Reviewed by Zero Degree on 12/10/2017 04:12:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.