Loading...

Zitto Kabwe afunguka kuhusu sakata la Airtel


Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameshauri kutazamwa mchakato mzima wa ubinafsishaji kwa kufanya ukaguzi maalumu wa sera ili kutoa mapendekezo ya kurekebisha makosa yaliyofanyika.

Amesema katika kufanya hivyo, suala la Airtel linaweza kushughulikiwa na kupata matunda mazuri zaidi.

Zitto katika taarifa kwenye mitandao ya kijamii leo Ijumaa Desemba 22,2017 amesema Serikali inaweza kuunda tume kutazama namna ubinafsishaji ulivyofanyika na kuchukua hatua za kisayansi baada ya matokeo ya kazi hiyo.

Amesema akiwa kiongozi wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) walifanyia kazi sera ya ubinafsishaji.

“Katika kila taarifa yetu ya mwaka tulikuwa na sehemu maalumu iliyoeleza ufuatiliaji wetu wa utekelezaji wa sera ya ubinafsishaji,” amesema. 

Zitto amesema ubinafsishaji wa iliyokuwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ni suala walilolitolea taarifa mara kadhaa bungeni na ya mwisho ilikuwa Januari 2015.

“Ni ukweli usio na shaka kuwa kampuni ya Celtel (sasa Airtel) haikulipa chochote kuwezesha kumiliki hisa kwenye Celtel Tanzania na pia uuzwaji wa Celtel kwenda Zain na kisha Airtel ulisababisha Tanzania kupoteza mapato ya kodi ya ongezeko la mtaji (capital gains tax),” amesema. 

Hata hivyo, amesema kunahitajika kushughulikia suala la Airtel kwa muktadha wa kazi nzima ya ubinafsishaji nchini.

Zitto amesema PAC iliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi baada ya ubinafsishaji wa mashirika kadhaa, ikiwemo Benki ya NBC na matokeo waliyawasilisha bungeni.

“Uuzwaji wa NBC nao ulikuwa ni wa bure na huwezi kushughulika na kampuni mojamoja bila kutazama muktadha mzima wa ubinafsishaji wa mashirika ya umma,” amesema.
Zitto Kabwe afunguka kuhusu sakata la Airtel Zitto Kabwe afunguka kuhusu sakata la Airtel Reviewed by Zero Degree on 12/22/2017 07:41:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.