Loading...

Magari ya kifahari bandarini yaanza kupigwa mnada

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere
MAGARI ya kifahari yaliyokwama kwa muda mrefu Bandari ya Dar es Salaam kutokana na waagizaji kushindwa kulipa kodi mbalimbali kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), yameanza kupigwa mnada huku kukiwa na dosari zilizofanya mnada usimamishwe kwanza.

Hata hivyo, wakati magari hayo yakipigwa mnada na Kampuni ya Yono Auction Mart ya Dar es Salaam, kasoro zimejitokeza kwenye mnada ikiwemo kutokuwepo kwa mazingira rafiki ya uuzwaji wa magari bandarini hapo.

Mwandishi wa habari hizi jana alishuhudia umati wa watu wapatao 3,000 ukiwa lango la kuingilia Bandari ya Dar es Salaam kuhudhuria mnada huo huku eneo la mnada likiwa dogo. Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere alikiri kuwepo kwa kasoro hizo na kusisitiza kuwa mnada ujao magari yatauzwa kwenye eneo kubwa la wazi Ubungo, ili wanunuzi wawe na fursa nzuri kuona magari yanayonadiwa.

Mnada huo uliendeshwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Yono Auction Mart, Scholastica Kevela ambaye amekuwa akiendesha minada mingine ya wadaiwa sugu wa kodi za TRA. Ukiondoa kasoro ya udogo wa eneo, baadhi ya wanunuzi waliojitokeza walilalamikia bei ya magari hayo kuwa kubwa zaidi kuliko sokoni. Mmoja wa wanunuzi, Mathew Mpanda alisema bei ya minadani huwa za kawaida lakini mnada wa safari hii ni ghali.

Kamishna Mkuu wa TRA, Kichere aliyekuwa akifuatilia uendeshaji wa mnada huo huku akizungumza na watu mbalimbali, baadaye alitoa tathimini yake kwa waandishi wa habari. Alisema licha ya kufurahishwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwenye mnada, kulikuwa na kasoro na akaahidi kuimarisha mnada ujao. Alisema mnada ujao watatoa fursa kwa kila mnunuzi kuyaona na kuyakagua magari kwanza, pia siku ya mnada wanunuzi watakuwa na fursa nzuri zaidi kufuatilia mnada na kushiriki vizuri.

Alisema awamu ya kwanza ya mnada imelenga kuuza magari 134 kati ya magari yote 600 yaliyolengwa kupigwa mnada huku akiweka wazi kama magari hayo ya jana 134 hayataisha, mnada utaendelea siku nyingine hadi yaishe. Pia alisema ili kuwapatia nafasi wafanyakazi wa ofisi za umma na binafsi kushiriki kwenye mnada huo, mnada ujao utafanyika Jumamosi na Jumapili ili waweze kuhudhuria kwa wingi.
Magari ya kifahari bandarini yaanza kupigwa mnada Magari ya kifahari bandarini yaanza kupigwa mnada Reviewed by Zero Degree on 1/05/2018 06:34:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.