Loading...

Vituo vitano vya Runinga vimepigwa faini na TCRA kwa kukiuka maadili

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TCRA, Joseph Mapunda
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevipiga faini vituo vitano vya runinga nchini Tanzania kwa makosa ya kukiuka Kanuni za Huduma za Utangazaji, Maudhui za mwaka 2005.

Vituo hivyo vilivyopigwa faini ni ITV, Azam TV, Star TV, Channel Ten na EATV kufuatia vipindi vyao vya taarifa ya habari vilivyoruka tarehe 30 Novemba 2017 katika nyakati tofauti tofauti.

Adhabu hizo zimekuja baada ya vituo hivyo vya Habari kurusha tathmini iliyotolewa na Kituo cha Haki za Binadamu juu ya uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika katika kata 43 mwaka jana 2017.

Akifafanua adhabu hizo leo Januari 2, 2018. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TCRA, Joseph Mapunda amesema Vyombo vyote vya habari vilipewa nafasi ya kutoa utetezi wao kuhusu taarifa hizo walizotoa kabla ya Mamlaka hiyo kutoa adhabu leo.

Makosa yote yaliyovikumba vituo hivyo vya Runinga ni matatu ambayo ni Uchochezi, Kukiuka maadili ya uandishi wa habari na Habari zao kukosa mizania.

Habari zote zilizotolewa na vituo hivyo vya Runinga kuhusu tathmini ya Uchaguzi mdogo wa madiwani iliyotolewa na Kituo cha Haki za Binadamu zilieleza kuwa uchaguzi huo ulikuwa na vitendo na matumizi mabaya ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kukamatwa na kujeruhiwa kwa lengo la kuharibu na kuvuruga uchaguzi na kuwatia hofu wapiga kura.

Adhabu kwa vituo vyote vitano ni kama ifuatavyo hapa chini:

  • ITV
    Kituo cha runinga cha ITV, kimetozwa faini ya jumla ya Tsh milioni 15, kwa makosa matatu ikiwemo, kukiuka maadili ya uandishi na kutangaza habari za uchochezi na faini hiyo inapaswa kulipwa ndani ya siku 30.
  • Azam Two
    TCRA imekitoza faini ya TZS milioni 7.5 kituo cha runinga cha Azam Two, kwa makosa ya kutangaza habari za uchochezi, kutangaza habari ambazo hazikuzingatia maadili ya uandishi na kutozingatia mizania.
  • EATV
    Kituo cha runinga cha EATV, kimetozwa faini ya jumla ya Tsh milioni 15, kwa makosa matatu ikiwemo, kukiuka maadili ya uandishi na kutangaza habari za uchochezi kwenye kipindi chake cha Hot Mix cha tarehe 30 Novemba 2017.
  • Channel Ten
    TCRA imekitoza faini ya Tsh milioni 15 kituo cha Runinga cha Channel Ten, kwa makosa ya kutangaza habari ambayo haikuzingatia maadili ya uandishi, kutangaza habari za uchochezi, na kutozingatia mizania.
  • Star TV
    Kituo cha runinga cha Star TV cha jijini Mwanza, kimetozwa faini ya jumla ya Tsh milioni 7.5 kwa makosa matatu ikiwemo, kukiuka maadili ya uandishi na kutangaza habari za uchochezi.
TCRA imesema adhabu zote za faini zinapaswa kulipwa ndani ya siku 30 na vituo vyote vilivyotoa taarifa hizo za kichochezi vitakuwa chini ya uangalizi maalumu wa TCRA kwa miezi 6.
Vituo vitano vya Runinga vimepigwa faini na TCRA kwa kukiuka maadili Vituo vitano vya Runinga vimepigwa faini na TCRA kwa kukiuka maadili Reviewed by Zero Degree on 1/02/2018 07:43:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.