Loading...

Vyama kususa uchaguzi ni kuwanyima haki wananchi - Prof. Lipumba

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kitendo cha baadhi ya vyama vya siasa kususa uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Longido mkoani Arusha na maeneo mengine nchini ni kuwanyima haki wananchi, kwa kuwa kufanya hivyo ni sawa na kumsusia nguruwe shamba la mihogo.

Profesa Lipumba alisema hayo juzi katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Longido mjini wakati akimnadi mgombea ubunge wa chama hicho, Kisiyongo Meseyeki Ole Kurya ili achaguliwe kuwa mbunge wa jimbo hilo. Alisema kitendo cha kususa uchaguzi kilichofanywa na baadhi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba mpya (Ukawa) ulifanywa kwa kukurupuka na ni kuiminya demokrasia ya vyama vingi.

Mwenyekiti huyo alisema CUF iliposhiriki uchaguzi kwa mara ya kwanza mwaka 1995 haikufanikiwa kupata kiti hata kimoja cha ubunge Tanzania Bara lakini kamwe hawakuweza kususa uchaguzi wa mwaka 2000 na ndio maana wameshiriki uchaguzi wa ubunge Longido na udiwani Arusha Mjini.

Alisema mwaka 2015 CUF ilishinda kwa kishindo uchaguzi Zanzibar lakini ukachakachuliwa na uliporudiwa chama hicho kilisusa na matokeo yake walipoteza viti vyote vya uwakilishi na ubunge Zanzibar na kuanza kujilaumu kwa kususa bila kuangalia mambo ya msingi.

Profesa Lipumba alisema kususa kwa Ukawa katika chaguzi za Longido na kwingineko ni sawa na mkulima kulisusia shamba la mihogo kwa nguruwe kwani athari yake ni kutaka bidhaa hiyo iendelee kuliwa na nguruwe na ndio maana Chama Cha Mapinduzi(CCM) kinafurahia hilo kama vile nguruwe alivyoachiwa shamba.

Alisema demokrasia ya kweli haitafutwi kwa kususasusa ila hutafutwa kwa mikiki ya kushiriki chaguzi zote zinazotangazwa na Tume ya Uchaguzi(NEC) na kutoa salamu kwa wananchi kuwa haki haiko sawa kwa wote kwa kuwaeleza katika mikutano ya hadhara ya kampeni.

Mwenyekiti huyo alisema kutafuta demokrasia ndani ya vyama kunahitaji mchakato wa muda mrefu na mchakato huo unahitaji uvumilivu na ujasiri mkubwa na sio kususa kwani watanzania watashindwa kuvielewa vyama vya siasa vya upinzani kama vitaendelea kususa chaguzi mbalimbali hapa nchini.

Alisema na kukiri kuwa ni kweli demokrasia hapa nchini ina mapungufu tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi, hivyo aliwataka viongozi wa vyama vya upinzani kuacha kususia uchaguzi kwani sio suluhisho la kudai Demokrasia kwani kususa ni kupotea kwa vyama hivyo na CCM kuendelea kutawa nchi.

Akizungumzia mapambano ya rushwa, ufisadi na kulinda rasilimali za nchi, Profesa Lipumba alisema kuwa kampeni hiyo ilianzishwa na Dk Wilbrod Silaa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema na alitaja orodha ndefu ya ‘mapapa na manyangumi’ katika uwanja wa Mwembe Yanga Temeke, Dar es Salaam, lakini Ukawa mwaka 2015 walimteua kiongozi mmoja aliyekuwa katika orodha hiyo kuwa mgombea urais, kitu ambacho upinzani ulipopoteza dira na mwelekeo wa mada nzima ya hilo na kushindwa hadi leo kulisemea hilo hadharani.

Profesa Lipumba alisema kwa uamuzi huo uliofanywa na Ukawa ulikuwa usaliti mkubwa kwa Dk Silaa kwani upinzani ulisifika kwa wananchi na kukubalika na kuonekana kuwa vyama vya upinzani viko tayari kukomboa wananchi kwa kupiga vita rushwa, ufisadi na kulinda rasilimali za nchi lakini sasa inakumbatia vita hivyo kwa kuwakubali wabadhirifu wa rasilimali za nchi.

Alisema kwa sasa Rais John Magufuli anafanya vizuri katika mapambano hayo na wananchi wanamkubali kwa kuchukuwa hatua bila ya kuangalia sura au chama kwani wote wanaohusika na matendo hayo wanachukukiwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Akimzungumzia mgombea wa CUF jimbo la Longido, alisema ni mgombea safi mkazi wa kijijini anayejua vilivyo changamoto za wakazi wa jimbo hilo, ikiwa ni pamoja na maji safi na salama kwa binadamu, maji kwa mifugo, elimu na miundombinu ya barabara.

Lipumba aliwataka wakazi wa Longido kufanya mabadiliko ya kumchaguwa mgombea wa CUF, Ole Kurya kwani ndio suluhisho la changamoto zote za wakazi wa Longido bila ya kujali itikadi zao za vyama. Naye mgombea ubunge wa CUF , Kisiyongo Maseyeki Ole Kurya aliwaomba wakazi wa Longido kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura kwani uchaguzi utakuwa wa amani na bila ya kusita wampe kura yeye kuwa mbunge wa jimbo hilo.
Vyama kususa uchaguzi ni kuwanyima haki wananchi - Prof. Lipumba Vyama kususa uchaguzi ni kuwanyima haki wananchi - Prof. Lipumba Reviewed by Zero Degree on 1/06/2018 09:40:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.