Loading...

Hakimu aliyemuhukumu Sugu aenda likizo


Hakimu Michael Mteite aliyemhukumu kifungo cha miezi mitano jela mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ameanza likizo jana.

Mteite, ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, alitoa hukumu hiyo juzi kwa Sugu pamoja na katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga baada ya kuwatia hatiani kwa kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Sugu na Masonga walitoa kauli hiyo Desemba 30 mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Hakimu huyo alipopigiwa simu jana na mwandishi wa Mwananchi aliyetaka kujua kuhusu uwepo wake likizo, kabla hata ya kuelezwa hilo alimtaka kuwasiliana na Msajili wa Mahakama.

Hata alipotumiwa ujumbe wa maneno (sms) kujulishwa kwamba msajili alishalizungumzia hilo na kilichohitajika ni kauli yake, hakujibu.

Awali, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, naibu msajili mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, George Herbert alisema Hakimu Mteite amechukua likizo kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa utumishi kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma pindi muda wao unapokuwa umefika.

“Ni likizo yake ya mwaka… na amechukua likizo kama mtumishi mwingine ambaye anaweza kuchukua likizo muda wake unapokuwa umefika. Kimsingi ni kwamba amechukua likizo ya muda wa wiki tatu kuanzia leo (jana) na ni likizo huwa anachukua kila mwaka muda unapokuwa umefika. 

“Hivyo suala la kusema kwamba eti amechukua likizo kwa sababu ya hukumu aliyoitoa jana (juzi) haina msingi wowote, bali ni haki yake kuchukua likizo hiyo. Inapofika Februari kila mwaka huchukua likizo yake na huwa inategemea majukumu anayokuwa amepangiwa kuyafanya,” alisema naibu msajili. 

Zaidi soma Mwananchi
Hakimu aliyemuhukumu Sugu aenda likizo Hakimu aliyemuhukumu Sugu aenda likizo Reviewed by Zero Degree on 2/28/2018 06:51:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.