Loading...

NEC: Malalamiko ya Mbowe sio ya kweli bali yamejaa upotoshaji wa hali juu

Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefunguka na kudai malalamiko yaliyotolewa jana (Jumanne) na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe sio ya kweli bali yamejaa upotoshaji wa hali juu ambao haupaswi kufanywa na kiongozi kama yeye.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa tume hiyo, Kailima Ramadhani baada ya kupita siku moja tokea Mhe. Mbowe kuzungumza mbele ya waandishi wa habari kuwa Tume ya Uchaguzi iliwafanyia hujuma katika kutoka viapo vya Mawakala wao kwenye chaguzi ndogo za marudio Jimbo la Kinondoni na mambo mengine.

"Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijibu malalamiko kwa matakwa ya mtu anavyotaka kujibiwa bali inajibu hoja kwa mujibu wa matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni na maadili ya uchaguzi na maelekezo yote ambayo yapo kwa mujibu wa sheria. Kama majibu ya tume hayakuwafurahisha CHADEMA, tume inasisitiza kuwa walijibiwa kwa matakwa ya sheria na katiba sio matakwa ya Mkurugenzi wa uchaguzi, Tume, Chadema au chama chochote cha siasa", amesema Kailima.

Aidha, Mkurugenzi Kailima amesema Kanuni, Sheria, maelekezo na maadili ya uchaguzi yameweka utaratibu wa kushughulikia malalamiko na changamoto zinazotokea wakati wa uteuzi, kampeni ambako kuna kamati za maadili na jinsi ya kukata rufaa.

"Kwa masikitiko CHADEMA walitekeleza hatua moja tu katika vipengele hivyo wakati wa uchaguzi, kipengele walichotekeleza ni pale baadhi ya wagombea wao walipoenguliwa kugombea ndipo walifuata utaratibu kwa kuwasilisha rufaa kwa Tume ya Uchaguzi na tume ilipitia na ikawarudishia wagombea wao kwenda kugombea", amesisitiza Kailima.

Mkurugenzi Kailima ameendelea kufafanua

"CHADEMA walitaka wakati wa kampeni, Tume ifanye maamuzi kinyume cha maadili waliyoyasaini. Wakati wa kampeni kuna kamati za maadili ngazi ya jimbo ambayo mwenyekiti ni msimamizi wa uchaguzi na wajumbe ni kutokea vyama vyote vilivyosimamisha wagombea na ndio wanaofanya uamuzi. Chadema waliwasilisha malalamiko kwa tume badala ya kuwasilisha kwenye kamati hizo za maadili zinazosimamia malalamiko yote".

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani amemsihi Mbowe na chama chake wasome sheria za uchaguzi na kuzielewa na kumsisitizia kuwa tume ipo tayari kumpa elimu ya mpiga kura na kuzifahamu sheria hizo zake kwa mapana.
NEC: Malalamiko ya Mbowe sio ya kweli bali yamejaa upotoshaji wa hali juu NEC: Malalamiko ya Mbowe sio ya kweli bali yamejaa upotoshaji wa hali juu Reviewed by Zero Degree on 2/28/2018 06:58:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.