Loading...

Idara ya Uhamiaji yafichua hujuma zaidi sakata la pasipoti mpya za kielektroniki


SIKU chache baada ya Rais John Magufuli kufi chua namna Idara ya Uhamiaji ilivyozima ufisadi wa Sh bilioni 400, zilizolengwa kuhujumiwa kupitia zabuni ya utengenezaji wa pasipoti mpya za kielektroniki za kusafiria, idara hiyo imefichua hujuma zaidi.

Katika hujuma mpya, idara hiyo imeeleza kuwepo kwa kundi la wanasiasa linalotumiwa kufanya siasa chafu za kudhoofisha mchakato wa utoaji hati mpya za kielektroniki za kusafiria; na kuwataka kuacha kufikiria maslahi yao na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa. Hivi karibuni Rais Magufuli wakati akizindua hati mpya za kusafiria za kielektroniki, alisema kumekuwapo na wahujumu wa mchakato huo, ambao walipanga kufisidi Sh bilioni 400, bila mafanikio.

Rais alisema watu hao wenye nia ovu, walizunguka kila kona na kutumia kila njama kupiga vita mchakato wa pasipoti mpya za kielektroniki, wakidhani watafanikiwa kuihujumu serikali. Akizungumza katika mahojiano maalumu na Habari- Leo jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dk Anna Makakala alifichua njama mpya ya kuwepo kwa kundi la wanasiasa, wanaoendelea kutumika na watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha ili kufanya hujuma hizo kwa maslahi yao binafsi.

Kamishna huyo alisema ni vyema jamii ikatambua kuwa mchakato huo, umegubikwa na vita vya ‘vigogo’ wanaowatumia wanasiasa wasiokuwa wazalendo, ambao wamekubali kutumika kwa maslahi yao binafsi. Pamoja na hilo, Kamishna huyo alisisitiza kuwa hatua ya mafanikio ya matumizi ya hati hizo, hazitarudi nyuma kwa sababu ya kuwapo na taarifa zisizo sahihi, zenye lengo la kupotosha ukweli wa mchakato huo.

“Ni vyema jamii kuelewa kazi ya hati hizo ni kulinda usalama wa nchi yetu, hivyo Uhamiaji tutaendelea kudhibiti mipaka ya Tanzania na kulinda usalama wa nchi kwa kuwezesha jamii na raia wa kigeni kufuata taratibu katika utokaji, ukaaji na uingiaji wa kila mmoja,” alisema. Alisema kila nchi yenye kuhitaji maendeleo ni muhimu kutumia hati ya kusafiria ya kielektroniki ili kufikia mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

“Mabadiliko ya kidunia katika maendeleo yanatuonesha wazi kuwa Taifa hili limefikia kuwa na hati za kisayansi na kiteknolojia, hivyo katika hati mpya mtu yeyote hataweza kutumia ujanja au kughushi na kutumika kwa matumizi yasiyo sahihi,” alisema. Alisema anaamini idara hiyo, haitashindwa na wachache, wanaokubali kutumika kuhujumu mchakato huo kwa maslahi binafsi, kwa kuwa kushindwa kwa mchakato huo ni kupunguza hadhi ya usalama wa nchi.

“Pasipoti ndiyo kitu kinachotuwezesha kudhibiti wanaoingia nchini na kutoka, hiki ni kitambulisho cha raia sehemu yoyote duniani wenye Pasipoti za Tanzania ni mabalozi wa Tanzania. “Mfumo huu utawezesha kudhibiti ujanja wote unaotumika, kutakuwa na ‘chip’ na security features nyingi, sifa ya Taifa letu dunia imeharibika, lazima kufanya maamuzi kwa maslahi ya Taifa letu,” alisema.

Dk Anna alisema kufanikiwa kwa mradi huo wa e-Immigration kwa gharama ya dola za Marekani milioni 57, imekuwa mwiba kwa vigogo walioondolewa Uhamiaji na sasa wanahaha kwa aibu, wakidai kwamba gharama iliyotajwa ni kwa ajili ya mradi mmoja tu wa e-Pasipoti. “Ni wajibu wa kila Mtanzania kuwa macho na wale wote wanaotumiwa na mafisadi kwa ajili ya kuichafua serikali, kwa kuwa imezuia na kupambana na uhujumu uliotaka kujitokeza,” alisema.

Alisema hati hizo zitawezesha waliopotelewa na hati zao, kutumia mfumo wa kiteknolojia na kupakua App yake hata katika simu ya mkononi, hivyo kutambulika na kupewa msaada haraka kokote duniani. Alisema hati hiyo ina viwango vyote vya ubora wa kimataifa, na itatumika pia kama kitambulisho kwa nchi za Afrika Mashariki. Akizungumzia gharama za hati, alisema Sh 150,000 anayolipia mwananchi ni sawa Sh 15,000 kwa mwaka kwa miaka 10 tangu inapotolewa.

“Hatukufanya hilo kwa bahati mbaya, tena serikali tunalipia zaidi kwa kuwa Shilingi 150,000 iliyotolewa ndani ya miaka 10 ya matumizi ya hati hizo ni sawa na kila mwananchi analipia Sh 15,000 kwa mwaka na nyingine inaongezwa na serikali ili kufikia gharama za utengenezaji wake,” alisema.

Alisema anawashukuru wananchi wengi, waliojitokeza kutaka kubadili hati zao za awali na wanaoomba hati mpya na kuahidi kuwa idara hiyo, itaendelea kufanya kazi kwa uadilifu na umakini mkubwa ili isitumike kisiasa.

Alisema mkakati uliopo ni mradi huo kufanyika kwa awamu nne, ambapo baada ya uzinduzi, mchakato wa e-VISA utakuwa Februari hadi Juni, e-Border utaanza Juni hadi Septemba na e- Immigration kwenye Balozi zote nje ya Tanzania, utaanza Septemba hadi Desemba, mwaka huu. Alisema miradi yote minne, itatekelezwa kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 57 pamoja na kodi kwa awamu zote na hakuna malipo mengine yatakayoongezeka.
Idara ya Uhamiaji yafichua hujuma zaidi sakata la pasipoti mpya za kielektroniki Idara ya Uhamiaji yafichua hujuma zaidi sakata la pasipoti mpya za kielektroniki Reviewed by Zero Degree on 2/08/2018 10:25:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.