John Bocco ndiye mchezaji bora wa VPL kwa mwezi Januari
Mshambuliaji wa Simba, John Bocco |
Bocco ambaye pia ni nahodha wa Simba alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba na Awesu Awesu wa Mwadui kutokana na uchambuzi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana wiki hii kupitia ripoti za makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa.
Alitoa mchango mkubwa kwa Simba mwezi huo ikipata pointi tisa katika michezo mitatu iliyocheza na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi, huku mshambuliaji huyo akifunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za usaidizi wa bao.
Pia kiwango cha mshambuliaji huyo aliyecheza dakika zote 270 za michezo mitatu ya Simba mwezi huo kilikuwa juu karibu kila mchezo.
Kwa upande wa Okwi aliyecheza dakika 206 kati ya 270 ilizocheza timu yake, alitoa mchango mkubwa kwa Simba kupata idadi hiyo ya pointi na kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi, huku akifunga mabao manne. Simba iliifunga Singida United mabao 4-0,ikaifunga Kagera Sugar mabao 2-0 na kisha ikailaza Majimaji mabao 4-0.
Awesu aliingia katika hatua hiyo kutokana na kung’ara katika michezo ambayo Mwadui ilicheza mwezi huo, akiibuka Mchezaji Bora katika mchezo wao dhidi ya Yanga, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam uliomalizika kwa timu hizo kutofungana, pia aliibuka mchezaji bora wa mchezo wo dhidi ya Njombe uliofanyika Uwanja wa Mwadui, Shinyanga na timu hizo kufungana mabao 2-2.
Mshambuliaji huyo aliyecheza kwa dakika 322 kati ya 360 ilizocheza Mwadui alifunga bao moja na kuisaidia timu yake kupata pointi sita katika mechi nne ilizocheza mwezi huo, ikitoka sare tatu na kushinda moja, ikiendelea kubaki nafasi ya kumi.
Kutokana na ushindi huo, Bocco atazawadiwa tuzo, kisimbuzi cha Azam na fedha taslimu sh. milioni moja kutoka kwa Mdhamini Mkuu wa Ligi, Kampuni ya Vodacom Tanzania.
Wachezaji wengine ambao tayari wameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi wa VPL msimu huu na miezi yao katika mabano ni Okwi (Agosti), beki wa Singida United, Shafiq Batambuze (Septemba) na mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa (Oktoba).
Wengine ni kiungo wa Singida United, Mudathir Yahya (Novemba) na mshambuliaji wa Mbao FC ya Mwanza, Habibu Kiyombo (Desemba).
John Bocco ndiye mchezaji bora wa VPL kwa mwezi Januari
Reviewed by Zero Degree
on
2/11/2018 11:54:00 PM
Rating: