Loading...

Ni haki ya kila mwananchi kupewa nakala ya hukumu yake - Jaji Mkuu

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma
Jaji Mkuu wa Tanzania Prof Ibrahim Hamis Juma amewaagiza Mahakimu wote nchini kutoa bure nakala za hukumu kwa wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa Haki.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Mahakama za wilaya ya Uvinza na Kasulu mkoani Kigoma leo, Jaji Mkuu amewaambia Mahakimu hao kuwa endapo watakutana na kikwazo cha Sheria, au Kanuni katika kutekeleza agizo hilo wasisiste kumpelekea mapendezo yao.

Jaji Mkuu amefikia uamuzi huo kutokana na Maboresho ya Huduma za Mahakama yanayoendelea pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/16 hadi 2019/20).

Alisema ni haki ya kila Mwananchi aliyekuwa na kesi mahakamani kupatiwa nakala ya hukumu yake ndani ya siku 21 tangu kusomwa kwa hukumu hiyo au mapema iwezekanavyo mara baada ya kesi yake kutolewa hukumu. Nakala ya hukumu imekuwa ikilipiwa kiasi cha shilingi elfu kumi (10,000) kama gharama ya uandaaji wa nakala hiyo. Akizungumzia maboresho ya huduma za mahakama, Prof. Juma alisema Mahakama inao mpango wa kuanzisha Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) ili kutatua changamoto ya upungufu wa Mahakama kwenye baadhi ya Maeneo nchini ikiwemo mikoa ya Tabora na Kigoma. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Zaidi ya watanzania milioni 25 wako mbali na huduma za Mahakama.
Ni haki ya kila mwananchi kupewa nakala ya hukumu yake - Jaji Mkuu Ni haki ya kila mwananchi kupewa nakala ya hukumu yake - Jaji Mkuu Reviewed by Zero Degree on 2/27/2018 09:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.