Loading...

Mikoa 18 yaripoti kuvamiwa na viwavijeshi


Mikoa 18 hapa nchini imeripoti kuwepo kwa wadudu waharibifu wa mazao aina ya viwavijeshi hali inayozua hofu kwa wakulima hasa wa mazao ya chakula waliopo kwenye mikoa hiyo.

Hayo yameelezwa leo na Ofisa Kilimo wa Kitengo cha Afya ya Mimea kutoka Wizara ya Kilimo, Victoria Ngowo wakati akitoa taarifa ya wadudu hao wavamizi kwa maofisa kilimo wa wilaya tano.

Ngowo aliyemwakilisha katibu mkuu wa wizara hiyo amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo maofisa kilimo wa wilaya hizo kubaini uwepo wa viwavijeshi na namna ya kuwashirikisha wakulima kuwadhibiti kabla hawajaleta uharibifu mkubwa.

Amesema kuwa nia ya Serikali ni kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya chakula na mengine hasa katika kuelekea kwenye uchumi wa viwanda, hivyo kama wadudu hao hawatadhibitiwa mapema ipo hatari ya kuwepo kwa upungufu wa chakula nchini.

Aidha, amesema kuwa pamoja na mafunzo hayo kwa maofisa kilimo, lakini pia wakulima watapewa mafunzo ya namna ya kutambua mapema uwepo wa wadudu hao shambani kwa kutumia kifaa maalumu cha kuwatega na kutumia dawa inayoelekezwa na wataalamu wa kilimo.

Naye Ofisa Kilimo Mkuu kutoka wizara hiyo, Sergei Mutahiwa amesema viwavijeshi bado havijatambulika sana na wakulima, hivyo kwa sasa jitihada zinazofanywa ni kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya kutosha ya kuwatambua wadudu hao.

Akielezea namna viwavijeshi hao wanavyoshambulia, Mutahiwa amesema wanao uwezo wa kula mazao ya aina 80 yakiwemo ya nafaka na kwamba, tayari baadhi ya dawa zimeshafanyiwa majaribio na kuthibitika kwamba zina uwezo wa kuua wadudu hao wakiwa katika hatua ya kwanza hadi ya tatu ya ukuaji wao.

Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Shirika la Nzige Jangwani, Shirika la Kimataifa la Misaada la Marekani (Usaid), Shirika la Chakula Duniani (Fao) na Serikali huku wilaya zilizopata mafunzo zikiwa ni Iringa, Hanang, Kilosa, Mbeya na Moshi.


Mikoa 18 yaripoti kuvamiwa na viwavijeshi Mikoa 18 yaripoti kuvamiwa na viwavijeshi Reviewed by Zero Degree on 2/27/2018 09:45:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.