Loading...

Rais Kenyatta akutana na Raila Odinga

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na kiongozi wa muungano wa upinzani nchini humo, Raila Odinga
RAIS wa Kenya Uhuru Kenyatta amekutana na kiongozi wa muungano wa upinzani nchini humo, Raila Odinga, katika ofisi yake ya Jumba la Harambee, Nairobi,a mbapo viongozi hao kwa pamoja wamekubaliana kuunda taifa lenye umoja.

Wawili hao wamekubaliana kuundwe mpango wa pamoja wa kuangazia utekelezaji wa malengo ya pamoja ya viongozi hao wawili, ambao utazinduliwa rasmi karibuni.

Balozi Martin Kimani ataongoza kuundwa kwa mpango huo upande wa Rais Kenyatta naye mshauri wa Bw Odinga Paul Mwangi atawakilisha Bw Odinga, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na Bw Kenyatta na Bw Odinga baada ya mkutano huo.

Mkutano huo umefanyika muda mfupi kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson kuwasili nchini humo kwa ziara ya siku nne.

“Tumekubaliana tutawaleta pamoja wananchi na kujadiliana kuhusu matatizo yanayoathiri taifa letu na wananchi, na kuunda taifa lenye umoja na lililo imara ambapo hakuna raia anayehisi ametengwa,” alisema Rais Kenyatta baada ya mkutano huo.

“Tumekutana na ndugu yangu Kenyatta, tumeongea kwa kirefu na kukubaliana kwamba tunataka kuiunganisha Kenya iwe taifa moja. Mgawanyiko ambao umekuwepo tangu uhuru utakwisha na sisi tutembee pamoja,” alisema Raila Odinga katika hafla hiyo.
Rais Kenyatta akutana na Raila Odinga Rais Kenyatta akutana na Raila Odinga Reviewed by Zero Degree on 3/09/2018 05:19:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.