Ujenzi wa barabara ya juu Tazara wafikia 80%
Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Patrick Balozi aliyasema hayo jana wakati wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi na Sekretarieti ya ERB, walipotembelea mradi huo na kuangalia ujenzi unavyoendelea na jinsi wazawa walivyoshirikishwa. Alisema mradi huo hadi sasa ulitakiwa kukamilika kwa asilimia 79.52 kulingana na matarajio, lakini kwa sasa upo mbele ya matarajio na umekamilika kwa asilimia 80 hadi sasa.
“Baada ya kutembelea mradi huu tumeona jinsi watanzania wameshirikishwa ambapo zaidi ya wahandisi 20 wa Kitanzania wameshiriki katika mradi huo na pia vifaa vingi vya ujenzi vimechukuliwa hapa nchini isipokuwa nondo ndiyo zimeagizwa nje kutokana na uhaba wa hapa nchini,” alisema.
Balozi alisema, “Natoa mwito kwa wawekezaji nchini kwamba bado kuna nafasi kubwa ya kuwekeza katika viwanda vya nondo, kwa kuwa bado tuna miradi mingi tunayotarajia kuitekeleza na inahitaji nondo nyingi ambapo kwa sasa hapa nchini hazikidhi mahitaji.”
Alisema, barabara hiyo ikianza kutumika itapunguza tatizo kubwa la foleni. Alisema serikali ina mpango wa kujenga barabara nyingine nane kama hizo katika jiji hilo, ambazo kwa sasa zinafanyiwa upembuzi yakinifu. Alisema barabara hiyo ni ya kwanza nchini na imetengenezwa kwa mafanikio makubwa. Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wamesimamia mradi huo kwa ufanisi mkubwa na hivyo kutarajiwa kukamilika mapema zaidi ya muda uliopangwa ambao ni Oktoba 31.
“Mradi huu unapowahi kukamilika pia ni faida kwa serikali, maana unapochelewa gharama huongezeka, changamoto kubwa wakati wa ujenzi mkandarasi amesema ni jinsi ya kudhibiti magari wakati wa ujenzi kwa kuwa hii ni barabara inayopitisha magari mengi yanayoenda uwanja wa ndege na bandarini,” alisema.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Sumitomo Mitsui Construction Co. Ltd.
Ujenzi wa barabara ya juu Tazara wafikia 80%
Reviewed by Zero Degree
on
3/09/2018 12:29:00 PM
Rating: