Wachakachuaji korosho mikononi mwa IGP
Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alitoa kauli hiyo mjini Dodoma jana, baada ya kupokea Ripoti ya Tume iliyoundwa na serikali kuchunguza tuhuma hizo za kusafirisha korosho zilizochanganywa na kokoto kwenye kontena ambalo lilibainika huko nchini Vietnam. Waziri Tizeba alimwagiza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo,Mathew Mtigumwe kuchambua orodha ya wote waliotajwa kwenye ripoti hiyo kwamba walihusika kwa njia moja au nyingine majina yao yafikishwe bila kucheleweshwa kwa IGP.
“Wote waliotajwa kuanzia kwenye maghala Liwale, walisafirisha, ofisa wa serikali aliyefunga rakili (seal), katika mashine za ukaguzi, kwenye makontena na wengine wote, majina yao yafikishwe kwa IGP, na kusiwe na ucheleweshaji,” alisema. Dk Tizeba alisema vitendo hivyo vya kuchanganya korosho na kokoto, havijaanza leo ni vya muda mrefu, kwani hata katika Chama cha Msingi cha Pangatena mkoani Lindi, iliwahi kubainika baadhi ya magunia ya korosho yalikuwa yamechanganywa na mawe. Dk Tizeba alisema, tabia hiyo ya kinyama au udanganyifu, inafanywa na baadhi ya wafanyakazi ambao wana tamaa, wengine wanataka kuharibu biashara ya korosho ambayo ilikuwa imeanza kuwapa manufaa makubwa wazalishaji.
“Uchunguzi umebaini kwamba kokoto zilizokutwa ndani ya magunia si za Liwale au Nachingwea bali ni za mwambao wa Pwani, umbali wa kilometa zaidi ya 200 kutoka kwenye minada zilikokuwa zikipakiwa kwenye magunia,” alisema. Alisema kitu cha kushangaza ni kwamba kwa nini kokoto hiyo haikuonekana kwenye magunia kwenye ukaguzi wa maofisa wa serikali, kwenye mashine za kuchunguza, bandarini na kwenye kontena hilo, hadi yanakwenda kupatikana sokoni nchini Vietnam, hivyo ni wahusika wote zilimopita korosho lazima wajieleze.
Akizungumzia baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo iliyowasilishwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Kassim Mbofu alisema yapo mambo yanayohusisha wizara nyingine mfano ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Hayo atawasiliana na Waziri mwenye dhamana, Profesa Makame Mbarawa kumweleza kuhusika kwa wizara yake na namna ya kuboresha upungufu uliojitokeza.
Pia kuhusu masuala ya maghala ambayo yapo chini ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, atazungumza na Waziri wake, Charles Mwijage kuona namna gani masuala ya kuboresha udhaifu uliopo kwenye maghala. Dk Tizeba alisema pia atazungumza na Balozi wa Vietnam ili kukutana na wabunge wa nchi hiyo ambao wapo hapa nchini, ili kuwaeleza nini kilitokea na mkakati wa serikali wa kuchukua hatua ili kudhibiti vitendo hivyo visijitokeze tena.
Akizungumzia uchunguzi wa Tume hiyo, Makamu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mbofu alisema tume ilifanya kazi kati ya Februari 5 hadi Machi 2, mwaka huu, na katika uchunguzi huo walibaini kwamba kontena hilo lilitoka Tanzania kutokana na takwimu zilizopo kwenye vituo lilimopita.
Mbofu alisema walibaini kwamba lilitoka Tanzania kutokana na viashiria mbalimbali vikiwemo vya magunia, namba ya uchunguzi wa ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika jengo la zamani na Nasaco, namba ya kontena iliyobeba kutoka Kampuni ya Kimataifa inayoshughulikia Upakuaji wa Makontena ya Mizigo Bandarini (TICS) na vingine vingi. Mbofu alisema katika uchunguzi huo, pia walifanya mahojiano na wadau mbalimbali wa korosho katika mkoa wa Pwani, Lindi na Mtwara na katika bandari ya Dar es Salaam hasa bandarini Dar es Salaam, wote walibainisha kwamba korosho hizo ni mali ya Tanzania.
Wachakachuaji korosho mikononi mwa IGP
Reviewed by Zero Degree
on
3/23/2018 01:40:00 PM
Rating: