Loading...

Serikali kudhibiti ubora wa elimu


SERIKALI imesema kuwa haitaruhusu kila mmiliki wa shule kujiamulia jinsi ya kudhibiti ubora wa elimu, kwani sio kila mwenye shule binafsi amekuwa akitumia uhuru huo vizuri.

Pia serikali imesema itaendelea kujadiliana na umoja wa wamiliki wa shule binafsi namna ya kuboresha utoaji elimu bila kuvunja sheria.

Aidha, hadi sasa serikali imeweza kuondoa tozo ya uendeshaji ujuzi, zimamoto, usalama mahali pa kazi na kodi ya mabango kwa shule hizo.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema). Selasini alitaka kujua serikali haioni sasa ni wakati wa kuziacha shule hizo zijiendeshe kwa taratibu zao kuweka viwango vya ufaulu.

Akijibu swali hilo, Waziri Ole Nasha alisema serikali itaendelea kuwaruhusu kuboresha utoaji elimu lakini bila kuvunja sheria na taratibu.

“Udhibiti wa ubora ni suala la kisera na kisheria hivyo Serikali haiwezi kuruhusu kila mmoja kudhibiti ubora katika shule yake,” amesema Ole Nasha.

Alisema wataendelea kujadiliana nao kuangalia namna ya kuwa na ada zinazohimilika zaidi. Katika swali la msingi, Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga aliuliza serikali haioni ni wakati muafaka kuondoa kodi zisizo na tija ambazo ni kero kwa shule za binafsi.

“Je, serikali haioni ni wakati sasa wa kuzipatia ruzuku shule binafsi kwa sababu zinashirikiana na serikali kupunguza tatizo la ajira,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo alisema serikali imekuwa ikishirikiana na wamiliki wa shule binafsi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo kodi na tozo.

“Katika kutatua changamoto hizo, hadi sasa serikali imeweza kuondoa tozo ya uendeshaji ujuzi, tozo ya zimamoto, kodi ya mabango na tozo ya usalama mahali pa kazi,” amesema.

Alisema hatua hiyo ya serikali ni kuhakikisha sekta binafsi inakuwa na mazingira rafiki na wezeshi kuwaletea Watanzania maendeleo.

“Hivyo, serikali kwa kushirikiana na umoja wa wamiliki wa shule binafsi itaendelea kujadiliana na kutatua changamoto zinazowakabili kuvutia uwekezaji katika sekta ya elimu,” amesema.

Alisema hadi sasa shule za msingi za binafsi zipo 1,432 kati ya 17,583 na za sekondari ambazo ni sekta binafsi ni 1,250 kati ya 4,885. Alisema serikali itaboresha taasisi za fedha ili sekta binafsi ipate mtaji kwa gharama nafuu.
Serikali kudhibiti ubora wa elimu Serikali kudhibiti ubora wa elimu Reviewed by Zero Degree on 4/24/2018 04:24:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.