Loading...

Serikali kulinda haki ya watanzania walioajiriwa nje ya nchi


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema italinda haki za Watanzania walioajiriwa katika nchi za Kiarabu kufuatia ripoti mbalimbali kuhusu kadhia wanazopata Watanzania hao ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa na kuteswa.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba alipokuwa akijibu swali la Mhe. Mgeni Jadi Kadika mbunge wa Viti Maalum CCM namna vijana wa Kitanzania hasa wa kike wanavyonyanyaswa wanapokwenda kufanya kazi za ndani katika nchi za Uarabuni.

“Nchi za Kiarabu zimekuwa zinatoa fursa nyingi za ajira katika kada mbalimbali kwa Watanzania na Serikali inapata faraja kuona vijana wake wanapata kazi hizo zinazowawezesha kuendesha maisha yao na familia zao. Hata hivyo, kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo wanaofanyia kazi, na haya yameonekana zaidi upande wa akina dada wanaokwenda kufanya kazi za ndani nchi za Kiarabu,” alisema Dkt. Kolimba.

Amesema, kufuatia ripoti mbalimbali kuhusu kadhia wanazopata Watanzania walioajiriwa katika nchi za Kiarabu. Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali kupitia Mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira ikiwemo Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) kwa kushirikiana na Wizara zinazoshughulikia masuala ya kazi na Ajira na Balozi zetu zilizopo nchi mbalimbali huko Mashariki ya Kati.

Aidha amesema, mikataba inayosainiwa na Waajiriwa hao pamoja na Waajiri wao inashuhudiwa na Balozi za Tanzania nchini humo ili kuhakikisha haki za Watanzania zinalindwa ipasavyo na hutakiwa kuripoti Ubalozini pale ambapo waajiri wao wanakiuka mikataba hiyo ikiwemo kunyanyaswa na kuteswa.

Hivyo basi mara baada ya balozi hizo kupokea taarifa za unyanyasaji huchukua hatua za mapema kuwasiliana na mwajiri pamoja na Mamlaka husika katika nchi hizo ili kusimamia na kutetea maslahi ya Watanzania.

Dkt. Kolimba amewataka Watanzania wanaoenda kufanya kazi nchi mbalimbali za Mashariki ya Kati kuhakikisha wanasaini mikataba hiyo kwani ina dhamira ya kuwalinda dhidi ya madhara yanayoweza kuwatokea kama ajali na majanga mengineyo.

Vile vile amesema, Serikali itaendelea kudhibiti Mawakala kwa lengo la kulinda maslahi ya Watanzania wanaochangamkia fursa za ajira katika nchi mbalimbali na hivyo kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Serikali kulinda haki ya watanzania walioajiriwa nje ya nchi Serikali kulinda haki ya watanzania walioajiriwa nje ya nchi Reviewed by Zero Degree on 4/06/2018 04:34:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.