Loading...

Hatimaye Kenya yarusha satilaiti katika anga za juu

Mfano wa Satelaiti ndogo
Kenya imetimiza ndoto kubwa ya kisayansi kwa kurusha setilaiti iliyoundiwa nchini humo.

Chombo hicho kilirushwa kutoka nchini Japan.

Chombo hicho kiliundwa na wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Nairobi kwa usadizi wa wataalamu kutoka Japan.

Wanasayansi wa anga za juu kutoka Kenya waliokiunda chombo walikuwa katika makao ya Uchunguzi wa Sayansi ya Anga za juu nchini Japan, (JAXA) ambapo chombo hicho kilirushwa kutoka huko.

Nchini Kenya kwenyewe raia walifuatilia shughuli hiyo moja kwa moja kwenye mtandao wa YouTube, na sherehe maalumu ya kushuhudia iliandaliwa katika chuo kikuu cha Nairobi.

Satelaiti hiyo ndogo ni ya thamani ya dola milioni moja - gharama inayoonekana kuwa ndogo kifedha kwa kiwango cha sayansi ya anga za juu.

Imebandikwa kamera mbili pamoja na vyombo vya kunasa na kupeperusha sauti.

Wahadhiri wa vyuo vikuu wanasema satelaiti hiyo inaweza kutoa huduma tofuati ikiwemo kukusanya taarifa zitakazosaidia katika kilimo na usalama, kutabiri hali ya hewa na hata kukabiliana na majanga.

Kenya kwa sasa inakabiliwa na janga la mafuriko ambalo limesababisha maafa makubwa.

Takriban watu mia mbili wamepoteza maisha yao, huku wengine zaidi ya laki mbili wamepoteza makaazi yao.

Huenda ufanisi katika uzinduzi wa satelaiti hii utaisaidia serikali pakubwa katika kujitayarisha kupambana na majanga ya aina hiyo.

Uzinduzi wa satelaiti hiyo leo unatokana na ushirikiano kati ya Idara ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, afisi ya masuala ya anga za juu ya Umoja wa Mataifa, na Shirika la utafiti wa anga za juu la Japan.

Kenya itaanza kushughulika kuunda satelaiti kubwa na bora zaidi baada ya uzinduzi wa leo kufanikiwa.
Hatimaye Kenya yarusha satilaiti katika anga za juu Hatimaye Kenya yarusha satilaiti katika anga za juu Reviewed by Zero Degree on 5/11/2018 05:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.