Loading...

Neema yazidi kumwagwa Simba SC


WACHEZAJI walioikacha Simba msimu huu na kutimkia kwingine, wanaweza wakajisikia vibaya sana watakapopata taarifa hizi kwamba baada ya wenzao kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, neema imewashukia.

Simba ambao mara yao ya mwisho kutwaa ubingwa ilikuwa msimu wa 2011/12, walikuwa wakipitia kipindi kigumu sana kuanzia msimu huo huku wakichekwa na wapinzani wao lakini msimu huu umekuwa wa furaha kwao.

Taarifa za uhakika ambazo DIMBA Jumatano limezinasa zinadai kuwa, bilionea wao, Mohamed Dewji, amewaambia viongozi wasiguse hizo Sh milioni 80 za ubingwa na badala yake zote wapewe wachezaji ambao ndio waliovuja jasho na kuleta mafanikio hayo.

Mbali na hilo, pia Mfanyabiashara huyo maarufu ndani na nje ya nchi, amedai atatenga mkwanja wa maana kwa ajili ya kuboresha timu hasa kwenye usajili wa msimu ujao akilenga zaidi michuano ya kimataifa watakayoshiriki.

Wekundu hao wa Msimbazi wataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu ujao baada ya kutwaa ubingwa huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Mo Dewji, amesema hataki kikosi hicho kiishie katikati na badala yake ikiwezekana wafike fainali na kutwaa ubingwa.

Akitumia ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa facebook, Mo Dewji aliandika: “Ubingwa tumeshapata sasa akili na nguvu zetu ni kuhakikisha tunakuwa makini katika usajili wa timu kuelekea michuano ya kimataifa.”

Mbali na andiko hilo, kigogo mmoja ndani ya Simba alisema kuwa, Mo ana malengo makubwa ndani ya timu hiyo na kama mambo yatakwenda vizuri kikosi chao hicho kitakuwa tishio ndani na nje ya nchi.

“Kuna kila dalili hizo Sh milioni 80 za ubingwa wakapewa wachezaji, kwani Mo Dewji amesema kwa sababu wao ni wavuja jasho lazima waangaliwe kwa jicho la tatu, huwa yeye si mtu wa maneno sana bali vitendo.

“Amesema hata kwenye usajili atahakikisha anaongeza wachezaji wazuri kutokana na jinsi benchi la ufundi litakavyotaka, ambapo analenga zaidi michuano ya kimataifa ambayo Simba watakuwa wakiiwakilisha nchi Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema kigogo huyo.

Taarifa nyingine zinadai kuwa katika Mkutano Mkuu wa Wekundu hao wa Msimbazi utakaofanyika Jumapili ya wiki hii ambao unalenga mabadiliko ya katiba, utatoka na maamuzi mazito hasa ya namna ya kumkabidhi Mo timu akiwa kama mwekezaji.

Atakapokabidhiwa timu moja ya mambo ambayo atayafanya ni kuhakikisha viongozi wote wababaishaji wanapigwa chini, lengo likiwa ni kuingiza kikosi kazi kitakachoifanya klabu hiyo kujiendesha kisasa zaidi.

Kigogo huyo alisema baada ya kupitishwa kwa ajenda katika mkutano huo, kutakuwa na mabadiliko makubwa ikiwamo suala zima la kuhakikisha hakutakuwa na Kamati ya Utendaji na zaidi ya kuwepo kwa Bodi ya Wakurugezi itakayokuwa chini ya mwekezaji huyo.

Katika mkutano huo unaotarajiwa kuanza saa 3 asubuhi katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, ajenda zitakuwa ni kufungua mkutano, kusoma mapendekezo ya marekebisho ya maboresho ya katiba ya Simba Sports Club na kupokea na kupitisha/kutopitisha marekebisho/maboresho ya Katiba.

Source: Dimba
Neema yazidi kumwagwa Simba SC Neema yazidi kumwagwa Simba SC Reviewed by Zero Degree on 5/16/2018 12:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.