Loading...

Serikali yapongezwa kuunda mabaraza 97


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza serikali kwa kuanzisha mabaraza 97 ya ardhi na nyumba nchini hata hivyo imeshauri itimize malengo ya kuanzisha mabaraza katika wilaya zote nchini.

Serikali pia imeshauriwa kuchukua hatua kumaliza mgogoro wa kiuongozi uliopo katika Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ikiwa ni pamoja na kuteua Bodi na Menejimenti ya Shirika hilo.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo bungeni jana, Halima Bulembo alisema serikali inatakiwa kutekeleza malengo hayo kwa kuzingatia umbali, jiografia na uwingi wa migogoro iliyopo.

Hata hivyo, kamati hiyo ilishauri serikali itoe vibali vya ajira ili wizara iweze kuajiri wataumishi kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya uhaba wa rasilimali watu unayoikabili mabaraza 44 yaliyoanzishwa kati ya 97 yaliyopo.

"Aidha, fedha za kutosha zinatakiwa kutengwa ili kuyawezesha mabaraza haya kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kupunguza msongamano wa migogoro ya ardhi katika maneno mbalimbali hapa nchini," alisema.

Kuhusu NHC, kamati hiyo ilibaini kuwa kutokuwepo kwa Bodi na Menejimenti ya Shirika kunazorotesha utendaji wa shirika na kulipunguzia kasi ya utekelezaji majukumu yake.

Halima alisema, Kamati imeridhishwa na taarifa ya ukaguzi wa shirika uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) inayotoa taswira halisi ya hali ya shirika kuliko taarifa zilizokuwa zimesambaa.

"Kamati inaishauri serikali kukamilisha tathmini ya hali ya ukwasi wa shirika ili liruhusiwe kuendelea kukopa kwa ajili ya kuendeleza miradi yake," alisema na kuongeza.

"Pia kukamilisha maandalizi ya sera ya Taifa ya Nyumba na kutekeleza ahadi yake ya kukutana na wapangaji wa shirika wa muda mrefu hasa wastaafu ili kukamaliza mgogoro wa upangaji wao."

Kuhusu urasimishaji wa makazi, Kamati ilishauri serikali kuongeza kasi ya utoaji hati kwa kupunguza gharama za upimaji na waandaaji wa hati.

"Serikali ianzishe utaratibu bora na rahisi wa kulipia gharama za kupima na kimiliki ardhi na iongeze kasi ya upimaji na urasimsishaji makazi sambamba na kasi ya ongezeko la watu na ukuaji wa miji," alisema.

Mfumo uunganishaji wa taarifa za ardhi (ILMIS), kamati ilishauri kusambaza mfumo unganishi wa hifadhi taafira za ardhi kwa halmashauri zote nchini. Kamati ilishauri kwamba wizara ihakikishe inatoa fidia stahiki kwa ajili ya ardhi inayotwaliwa kwa ajili yamatumizi ya maendeleo inalipwa ipasavyo.

Source: Habari Leo
Serikali yapongezwa kuunda mabaraza 97 Serikali yapongezwa kuunda mabaraza 97 Reviewed by Zero Degree on 5/30/2018 08:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.