Loading...

Watu zaidi ya 100 wafariki dunia kwenye ajali ya ndege

Mabaki ya ndege hiyo iliyoanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Jose Marti
Watu zaidi ya 100 wamefariki dunia baada ya ndege ya kuwabeba abiria aina ya Boeing 737 kuanguka na kulipuka karibu na uwanja mkuu wa ndege wa Cuba mjini Havana, katika mkasa mbaya zaidi wa ndege nchini humo katika miongo kadha.

Wanawake watatu waliondolewa kutoka kwenye mabaki ya ndege hiyo wakiwa hai, lakini taarifa zinasema wamo hali mahututi.

Ndege hiyo, ambaye iliundwa karibu miaka 40 iliyopita, ilikuwa imewabeba abiria 104 na wahudumu sita wa ndege.

Serikali ya Cuba imeanzisha uchunguzi, na kutangaza siku mbili za maombolezo ya kitaifa.

Ndege hiyo Boeing 737-201 ilianguka saa sita na dakika nane mchana Ijumaa, muda mfupi baada ya kupaa kutoka Havana.

Ndege hiyo ilikuwa kwenye safari ya ndani ya nchi kutoka Havana kwenda Holguin, mashariki mwa Cuba.

Wahudumu wote sita wa ndege hiyo walikuwa raia wa Mexico lakini wengi wa abiria ni raia wa Cuba.

Taarifa zinasema kulikuwa na abiria watano raia wa kigeni.

"Kumekuwa na ajali ya ndege ya kusikitisha sana. Taarifa tulizo nazo ni za kutamausha, yamkini kuna idadi kubwa sana ya waathiriwa," Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel alisema baada ya kutembelea eneo la ajali.

Ni mapema sana kubaini chanzo cha ajali hiyo, lakini walioshuhudia kutoka ardhini wanasema ndege hiyo ilishika moto kabla ya kuanguka katika eneo wazi lililo karibu na msitu mbogo karibu na uwanja huo wa ndege wa Havana.

"Niliiona ikipaa," mfanyakazi wa duka la jumla Jose Luis aliambia shirika la habari la AFP.

"Ghafla, iligeuka na kuanguka. Tulishangaa sana."

"Tulisikia mlipuko mkubwa na kisha tukaona wingu la moshi ukitanda angani," Gilberto Menendez, ambaye ana mgahawa karibu na eneo la mkasa ameambia Reuters.

Idara ya uchukuzi ya Mexico imesema kwenye tovuti yake kwamba "wakati wa kupaa, ndege hiyo yamkini ilipata hitilafu za kimitambo na ikaanguka."

Boeing wamesema watatuma kundi la mafundi wake Cuba, "kama inavyoruhusiwa chini ya sheria za Marekani na kwa uelekezi wa Bodi ya Taifa ya Usalama katika Uchukuzi ya Marekani na maafisa wa serikali ya Cuba."

Kumekuwepo na vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Cuba kwa miongo mingi.

Watu wanne walinusurika ajali hiyo lakini mmoja alifariki akisafirishwa kupelekwa hospitalini, mkurugenzi wa hospitali ya Calixto Garcia mjini Havana, Carlos Alberto Martinez, ameambia Reuters.

Manusura hao watatu wote ni wanawake, kwa mujibu wa gazeti la Chama cha Kikomunisti cha Cuba, Granma.

Mmoja umri wake ni miaka 18 hadi 25, wa pili ana miaka 30 hivi na mwingine ana miaka 39.

"Yuko hai lakini amechomeka sana na moto," jamaa wa mmoja wa wanawake hao aliambia Reuters katika hospitali hiyo.

Serikali za Argentina na Mexico zimethibitisha kwamba raia wa mataifa hayo mawili ni miongoni mwa waliofariki.

Ndege hiyo ilikuwa imekodishwa kwa shirika la taifa la ndege la Cuba, Cubana de Aviación na kampuni ya uchukuzi wa ndege ya Mexico, Aerolineas Damojh.

Maafisa wa Mexico wanasema ndege hiyo iliundwa mwaka 1979 na ilikaguliwa na kubainika haikuwa na kasoro yooyte Novemba mwaka jana.

Mexico imesema inawatuma wataalamu wawili wa masuala ya uchukuzi wa ndege kushiriki katika uchunguzi.

Aerolineas Damojh, shirika ambalo pia hufahamika kama Global Air, lina ndege tatu ambazo bado zinafanya kazi.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka kwa sekta ya uchukuzi wa ndege, mwaka jana uliokuwa miongoni mwa miaka salama zaidi katika uchukuzi wa ndege za kubeba abiria, lakini mwaka huu kumekuwa na ajali kadha kubwa.

Mwezi jana, ndege ya jeshi ilianguka muda mfupi baada ya kupaa Algeria, na kuwaua watu zaidi ya 250.

Februari, ndege ya shirika la Saratov Airlines ilianguka karibu na Moscow na kuwaua watu 71.

Na mwezi Machi, ndege ya shirika la US-Bangla Airlines ilianguka Kathmandu, Nepal; watu 51 walifariki.

Ajali mbaya zaidi ya ndege Cuba ilitokea mwaka 1989, ndege iliyoundiwa Muungano wa Usovieti aina ya Ilyushin-62M ilipoanguka karibu na Havana na kuwaua watu 126 waliokuwa ndani ya ndege hiyo, na wengine 24 ardhini.
Watu zaidi ya 100 wafariki dunia kwenye ajali ya ndege Watu zaidi ya 100 wafariki dunia kwenye ajali ya ndege Reviewed by Zero Degree on 5/19/2018 08:50:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.