Loading...

Serikali kudhibiti Ajira kwenye maeneo nyeti


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali inadhibiti raia wa nje wasipate ajira kwenye maeneo ya usalama kama bandari, viwanja vya ndege na mipakani ili kulinda usalama wa nchi.


Sambamba na hilo, amesema Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura), wameanza ukarabati wa miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini. 

Akizungumzia ajira za wageni katikia maswali ya papo kwa hapo bungeni jana, Majaliwa alisema; “Kwa sasa tunaendelea kudhibiti maeneo hayo ya usalama na hakuna mgeni anafanya kazi huko.


“Hata ukikuta mgeni ameajiriwa na kampuni, basi jua kuwa kutakuwa hakuna Mtanzania mwenye sifa ya kazi anayoifanya, tunasimamia sana hili hakuna ujanjaujanja.” Alisema ajira za wageni zimeruhusiwa katika nafasi za kitaaluma tu ambazo Watanzania hawana utaalamu nazo. Hata hivyo alisema katika taasisi moja inaruhusiwa kuwa na wageni wasiozidi watano. “Ofisi yangu inaendelea kusimamia hili ili Watanzania wapate fursa na tunadhibiti wageni wasichukue ajira hizi,” alisema.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Leah Komanya (CCM) aliyetaka kufahamu kama serikali inadhibiti maeneo ya usalama wa nchi kama bandarini, uwanja wa ndege na mipakani ili wageni wasiajiriwe kwani kwa sasa kuna wimbi kubwa la wageni kupata ajira nchini. Kuhusu athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini, Waziri Mkuu alisema tayari Tarura na Tanroads wameanza kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na mvua hizo.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) aliyetaka kufahamu hatua iliyochukuliwa na serikali kurejesha mawasiliano ya miundombinu iliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha, ambapo alisema baadhi ya mikoa imeshafanya tathmini ya uharibifu huo kwa miezi miwili sasa.
Serikali kudhibiti Ajira kwenye maeneo nyeti Serikali kudhibiti Ajira kwenye maeneo nyeti Reviewed by Zero Degree on 5/19/2018 09:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.