Loading...

Pacha waliouangana Maria na Consolata wazikwa mkoani Iringa


Watu wengi walijitokeza Iringa kuwaaga pacha waliokuwa wameungana Maria na Consolata waliofariki mwishoni mwa juma.

Miongoni mwa waliofika ni viongozi mbali mbali wa dini na kiserikali, akiwemo waziri wa elimu Prof Joyce Ndalichako.Pacha hao walizikwa katika makaburi ya Tosamaganga baada ya ibada ya wafu kufanyika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCU).

Askofu Jimbo Katoliki Njombe, Alfred Maluma amesema vifo vya Pacha hao vinafaa kutumiwa na Watanzania kukumbushana wajibu wao kwa watu wenye ulemavu.

"Wameacha somo hilo, tuwajali watu wenye ulemavu hilo ndilo somo walilotuachia Maria na Cobsolata."

Amesema Mungu aliwaumba pacha hao kwa mfano wa sura yake na akawapa uhai kwa kipindi walichokuwa duniani.


Vifo vya Maria na Consolata ambao walikuwa ni wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Ruaha vimegusa wengi hasa kutokana na ujasiri walioonyesha wakati wa uhai wao.

Pacha hao wameandaliwa jeneza moja lenye mfumo wa watu wawili, misalaba miwili na watazikwa katika kaburi moja.

Mkuu wa Shirika la Maria Consolata, Jane Nugi alikuwa ameambia gazeti la Mwananchi kwamba pacha hao waliamua eneo ambalo watazikwa.

Alisema katika uhai wao walichagua kuzikwa kwenye eneo wanalozikwa viongozi wa kanisa Katoliki eneo hilo.

"Wakati wakiumwa walisema wangetamani kuhifadhiwa tunakohifadhiwa sisi hivyo watazikwa kwenye makaburi ya Tosamaganga," alisema.

Pacha hao walifariki dunia wakiwa katika hospitali ya Iringa usiku wa kuamkia Jumamosi.

Kifo chao kiliwagusa wengi Tanzania, wengi wakituma salamu zao za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii.

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli, ambaye mapema mwaka huu alikutana na pacha hao, alieleza kusikitishwa kwake na vifo vyao.

"Nimesikitishwa na kifo cha Maria na Consolata. Nilipokwenda hospitali waliliombea taifa. Walikuwa na ndoto ya kulitumikia taifa," aliandika Rais Magufuli kwenye Twitter.

Maisha ya Maria na Consolata
Maria na Consolata Mwakikuti walizaliwa eneo la Ikonda, wilaya ya Makete kusini magharibi mwa Tanzania mwaka 1996.

Walisoma shule ya msingi ya Ikonda kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Maria Consolata na baadaye wakasomea hadi kidato cha sita katika shule ya Udzungwa wilaya ya Kilolo.

Septemba mwaka jana, baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita, walijiunga na chuo kikuu cha kikatoliki cha Ruaha, Iringa.

Walianza kuugua maradhi ya moyo na Desemba wakahamishiwa taasisi ya maradhi ya moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako walilazwa kwa miezi miwili.


Walipofaulu mtihani wa kidato cha sita, walieleza furaha yao kuu baada ya kufaulu mtihani na kueleza ndoto zao.

"Tulipokea matokeo yetu tukiwa kwenye mazingira ya nyumbani tu, tukiendelea na shughuli zetu za kila siku, tukaambiwa matokeo yametoka na tumefanya vizuri, tulikuwa tukiwaza kabla ya hapo, unajua kwenye mitihani ya mwisho huwezi kujiamini sana," alieleza Consolata.


Walieleza sababu za kuchagua chuo cha Ruaha kwenye mkoa waliokuwa wanaishi tofauti na vyuo vingine au kama ilivyo kwa wanafunzi wengine ambao hupenda kubadili mazingira.

"Kwanza tunapenda mazingira ya Iringa, hatukutaka kwenda Dar es Salaam kwa sababu ya kwanza tunapenda kuishi pamoja na walezi wetu Masista waliokuwa wanatulea tukiwa wadogo na pili mikoa mingine ni mbali na tunapoishi. Pia ni kwa sababu kwa hali yetu tulivyo hatumudu kuishi kwenye mazingira ya joto. Mji wa Iringa ni baridi, hali hii tumeizoea.''


Walitaka kuolewa na mwanamume mmoja


Maria na Consolata walikuwa wamewahimiza wazazi kuwajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu wakisema hakuna lisilowezekana.

"Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na mtoto mlemavu ni laana. Pili wawaone kama watoto wengine na kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri.''
Pacha waliouangana Maria na Consolata wazikwa mkoani Iringa Pacha waliouangana Maria na Consolata wazikwa mkoani Iringa Reviewed by Zero Degree on 6/06/2018 01:50:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.