Hili ndilo gari la Mahakama inayotembea
Miongoni mwa changamoto zinazotajwa kuwapo katika mhimili wa mahakama nchini, ni mlundikano wa mashauri mahakamani. Inaelezwa kuwa baadhi ya kesi huchukua muda mrefu kwa kuwa wenye kesi hizo hukumbana na changamoto ya kutumia gharama kubwa kwa ajili ya usafiri kufika mahakamani hatua ambayo huwavunja nguvu na kutoona haja ya kuendelea nazo jambo linalowafanya wapoteze haki zao.
Tatizo hili sasa litapungua kama si kufikia ukingoni baada ya Mahakama ya Tanzania kuanzisha mahakama inayotembea ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Mpango huo unatarajiwa kuwa mkombozi wa wananchi hususani kwa wale wanaoshindwa kupata haki zao kwa sababu hiyo.
Mahakama inayotembea ni gari maalumu ambalo limeundwa kama chumba kilicho na huduma zote za kiofisi ambazo hakimu anazihitaji wakati wa kutekeleza wajibu wake wa kusikiliza kesi na kutoa hukumu.
Tanzania inatajwa kuwa nchi ya kwanza Afrika kuanzisha mahakama inayotembea itakayokuwa ikizunguka kuwafuata wananchi waishio maeneo yaliyo mbali na mahakana ili kuwapatia huduma kama zinavyotolewa katika mahakama nyingine.
Wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria yaliyofanyika wiki iliyopita, Rais John Magufuli alizindua magari mawili yatakayofanya kazi kama mahakama inayotembea ambayo kwa kuanzia yatatoa huduma mkoani Dar es Salaam na Mwanza huku lengo likiwa ni kuwa na magari ya aina hiyo nchini kote.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma anaielezea dhana ya mahakama inayotembea kuwa inalenga kusogeza huduma za kimahakama karibu na wananchi.
Anasema dhana hiyo ilikuwepo tangu mwaka 1920, mahakama ilikuwa ikitumia behewa la treni kwenda kusikiliza kesi maeneo yaliyokuwa yakifikiwa na usafiri huo. Sababu ya kuanzishwa mahakama hiyo ilikuwa ni kumfuata shahidi ambaye ama alikuwa mgonjwa au kufuata kielelezo kisicho hamishika kirahisi.
“Kwa sasa, mahakama inayotembea inamaanisha kusogeza huduma karibu na wananchi hasa sehemu zisizo na huduma ya mahakama kwa lengo la kusikiliza kesi na kuzimaliza.
“Mahakama itahamishia shughuli zake katika chumba maalumu chenye huduma zote muhimu,” anasema Profesa Juma.
Jaji Mkuu anasema wamenunua magari mawili yatakayotumika kama mahakama inayotembea ambapo katika awamu ya kwanza ya majaribio yatatoa huduma jijini Dar es Salaam na Mwanza.
Anasema kwa Dar es Salaam, magari hayo yatakuwa na vituo vifuatavyo; Kinondoni kituo kitakuwa Bunju, wilaya ya Ilala (Chanika), wilaya ya Temeke (Buza) na wilaya ya Ubungo (Kibamba).
Licha ya kwamba mlundikano wa kesi umepungua kwa kiasi kikubwa, Profesa Juma anasema mahakama hizo nazo zitasaidia kupunguza zaidi mashauri yasiyosikilizwa kwa muda mrefu kwenye mamlaka zake.
Anasema mwaka jana mahakama za mwanzo nchini zilisajili mashauri 176,652 na kusikiliza 175,572 ndani ya ukomo wa muda wa miezi sita na mashauri 15,675 yalibaki. Kwa upande wa mahakama za wilaya zilisajili kesi 51,161 na kusikiliza 47,089 ndani ya ukomo wa muda wa mwaka mmoja.
Profesa Juma anasema katika kuboresha huduma za mahakama wameanza pia kusikiliza mashahidi kupitia video (video conference), ili kupunguza gharama na muda wa usikilizaji kesi. Alitoa mfano Desemba 5, mwaka jana, Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara ilimsikiliza shahidi akiwa Ufaransa kupitia mfumo huo.
Muundo mahakama inayotembea
Profesa Juma anasema kwamba mahakama inayotembea ni gari maalumu lenye sehemu mbili; kwanza, chumba cha hakimu ambacho kina meza ya wadaawa, meza ya karani na televisheni.
Vitu vingine vilivyomo kwenye chumba cha hakimu ni kompyuta, printa, kabati la kutunzia majarada, vyombo vya kurekodia mashauri na vifaa vya kutangazia. Profesa Juma alitaja sehemu ya pili kuwa ni chumba cha faragha (choo).
Msimamizi wa moja ya magari hayo, Moses Ndelwa anasema kwamba magari hayo yameunganishwa na mfumo wa kuratibu mashauri mtandaoni, hivyo hakimu ataweza kupata mashauri yote akiwa ndani ya gari hilo.
Anasema mahakama inayotembea itafanya kazi kama mahakama ya mwanzo au ya wilaya na itahudumia watu katika eneo la mamlaka ya mahakama ambapo litakuwepo. Anasema kesi zitakazosikilizwa ni zile mpya au mashauri maalumu.
“Gari hili lina mambo yote muhimu kwa hakimu, ofisi imekamilika kumwezesha kutekeleza majukumu yake. Mbali na sehemu ya hakimu, kuna meza ya karani, meza ya wadaawa, vifaa vyote vya ofisini na choo pia,” alisema Ndelwa.
Baadhi ya wanasheria waliipongeza Serikali kwa kuanzisha chombo hicho wakisema kitasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri na kuhamasisha wananchi kupeleka mbele ya mahakama malalamiko yanayohusu kudai haki zao.
“Huko mitaani au vijijini kuna migogoro mingi ambayo haijafikishwa mahakamani. Wananchi wanaamua kuimaliza wenyewe kwa sababu ya umbali uliopo kuzifikia mahakama au usumbufu ambao hukutana nao. Sasa wakiiona mahakama hii kwenye maeneo yao watahamasika kupeleka mashauri yao ili yakapatiwe mwongozo na ufumbuzi wa kisheria,” anasema wakili wa kujitegemea, Emmanuel Chuma.
Wakili mwingine wa kujitegemea, Simon Ng’ingo anasema mahakama inayotembea ni hatua kubwa katika jitihada za kusogeza huduma kwa wananchi. Anasema elimu itolewe ili Watanzania wazione mahakama hizo kama zilivyo nyingine.
Wakati wa hotuba yake, Rais Magufuli alisisitiza umuhimu wa mahakama inayotembea katika kutatua matatizo ya wananchi hususani mirathi kwa wajane na kuitaka Benki ya Dunia (WB) ambao ndiyo iliyofadhili mradi huo kuongeza magari mengine ili angalau gari moja likashughulikie mirathi.
“Wajane wanapata shida sana, mtu anafiwa na mume wake wanaochukua mirathi wanachukua hata kama si wahusika. Naomba hili mkaliangalie ili haki za wajane hawa ziende zikasikilizwe. Hata kama ni kuamua kuwe na timu au kuwe na mobile court (mahakama inayotembea) ya kushughulikia wajane tu, iwe hivyo,” anasema Rais Magufuli.
Hili ndilo gari la Mahakama inayotembea
Reviewed by Zero Degree
on
2/11/2019 08:20:00 AM
Rating: