Mapori 5 kuwa hifadhi za Taifa
Pia serikali ipo katika kampeni ya kuchora upya ramani na vivutio mbalimbali vya utalii nchini kwa lengo la kuongeza, kubadili na kupanua vivutio vya utalii nchini.
Akiwahoji wabunge jana kabla ya kupitia azimio hilo bungeni, Spika wa Bunge, Job Ndugai alishangaa wabunge wote walivyokubaliana kuridhia azimio la kupandisha hadhi mapori hayo kuwa hifadhi za taifa.
Akihitimisha hoja za wabunge, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla alisema kwa Bunge kuridhia kupandisha hadhi mapori hayo, Taifa litapata manufaa yakiwemo ya kuimarisha uhifadhi wa maliasili hasa wanyamapori, mimea na mazalia na makuzio ya samaki na viumbe wengine kwenye maji.
Pia utaongeza Pato la Taifa kwa msingi ubadilishaji hadhi utasaidia hifadhi hizo kuwa vivutio vya utalii.
Alisema uhifadhi na usimamizi endelevu wa mapori haya ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kimazingira kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo. Usimamizi huo utawezesha kuondoa uharibifu wa mazingira, uvamizi wa mifugo, ujangili na uingizwaji wa silaha haramu za kivita.
Akisoma maoni ya kamati, Makamu wa Mwenyekiti, Timotheo Mnzava alisema uamuzi wa kupandisha hadhi mapori hayo kuwa hifadhi za taifa utaimarisha ulinzi.
Alisema kamati inalishawishi Bunge kupitisha azimio hiyo kwani hatua hiyo itajenga mazingira bora kwa ajili ya kuendeleza utalii na kukuza pato la taifa.
Lakini inashauri ili kuepusha uwezekano wa hifadhi mpya kuwa na migogoro, kamati inashauri serikali kuhakiki mipaka husika kwa kushirikisha wananchi ili kuepuka kuwepo kwa migogoro ya mipaka.
Akitoa maoni yake, Mbunge wa Kuteuliwa, Salma Kikwete (CCM) alisema ni vema kupandisha hadhi mapori hayo na serikali inatakiwa kukumbuka na mikoa ya Kusini kwani Watanzania wote ni wamoja.
Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate (CCM), alisema kupandishwa hadhi kwa mapori kutapunguza tatizo la uhalifu kwani wenyeji wa Kagera walitakiwa kupita mapori hayo wakiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM) alisema kupandisha hadhi kutatoa faida ya kuongeza Pato la Taifa, kuongeza ajira na kuongeza watalii kupitia uwanja wa ndege wa Chato mkoani Geita.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwanko (CCM) alisema wakati wanapandisha hadhi mapori hayo wanatakiwa pia kukumba mapori ya Kigosi na Mayowosi kwani yapo katika ekolojia moja.
Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) alipongeza uamuzi wa kupandisha hadhi mapori hayo lakini akataka wasitelekeze mkakati wa kuboresha korido ya Kusini ambayo mradi wa uendelezaji ukanda huo ulishaanza.
Sasa kuna hifadhi 14, Serengeti, Ziwa Manyara, Arusha, Ruaha, Mikumi, Gombe, Tarangire, Kilimanjaro, Katavi, Rubondo, Milima Mihale, Udzungwa, Saadani, Kitulo, Mkomazi na Kisiwa cha Saanane.
Usimamizi wa maeneo ya wanyamapori unahusisha hifadhi za Taifa 16 zinazosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), mapori ya akiba 28 na mapori tengefu 42 yanayosimamiwa na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (Tawa).
Chanzo: Habari Leo
Mapori 5 kuwa hifadhi za Taifa
Reviewed by Zero Degree
on
2/11/2019 07:50:00 AM
Rating: