Loading...

Mahakama kuamua kesi vigogo 9 Chadema


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo itatoa uamuzi katika kesi ya uchochezi, inayowakabili vigogo tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kama iendelee kwa utetezi au iahirishwe, kwa sababu washitakiwa wawili wamepata safari nje ya nchi.

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa utetezi, ukiongozwa na Wakili Profesa Abdallah Safari kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kwamba wanaomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 7 na 8, mwaka huu, kwa sababu wanahitaji kupata muda wa kutosha kujiandaa na utetezi.

Alidai kuwa wanahitaji muda wa kutosha wa kujiandaa na utetezi, kwa kuwa wana mashahidi wengi ambao wanahitajika kutafutwa na kuandaliwa.

Hata hivyo, alidai kuwa mshitakiwa Dk Vincent Mashinji (Katibu Mkuu Chadema) yupo Songea na kwamba Septemba 26 mpaka Oktoba 6, mwaka huu atakuwa nchini Uingereza na mshitakiwa Ester Matiko (Mbunge wa Tarime Mjini) kuanzia Septemba 25 hadi 28, mwaka huu anatakiwa kwenda Kigali nchini Rwanda na Oktoba 13 hadi 18 atakwenda kuiwakilisha nchi barani Ulaya.

Baada ya maelezo hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alidai kuwa barua ya Mashinji haioneshi safari hiyo anayotarajia kwenda ni ya namna gani.

“Hicho tu hakijajitosheleza kiasi cha kuifanya mahakama kutoa uamuzi wa kuahirisha kesi, pia barua hiyo haielezi anakwenda huko kufanya nini na kwanini aende mshitakiwa huyo ambaye tarehe hizo shauri lake litatajwa ma hakamani”, alidai Nchimbi.

Kuhusu mshitakiwa Matiko, Nchimbi alidai barua ya mshitakiwa huyo, inaonesha imetoka Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla) kwenda kwa Katibu wa Bunge, wakiomba uwakilishi wa wabunge sita nchini Kigali.

Alidai hayo yanabaki kuwa maombi ambayo yanaweza kukubaliwa au kukataliwa ; na kuongeza kuwa hakuna sababu ya mshitakiwa huyo kwenda safari hiyo, kwa kuwa kuna uwakilishi wa wabunge wengine watano.

“Ni vema ifahamike kwamba mtuhumiwa anapokuwa na kesi ma hakamani ni wazi ratiba yake kiasi fulani itaingiliwa na taratibu za mahakama, kama itakuwa kila mshtakiwa akijisikia kusafiri anapatiwa ruhusa kwa vyovyote vile shauri hili halitafikia mwisho,” alidai Nchimbi.

Akijibu hoja hizo, Profesa Safari alidai kuwa safari za nje ya nchi, haziwezi kuwa za kienyeji na washitakiwa hao hawawezi kuidanganya mahakama.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Simba alisema leo atatoa uamuzi kama kesi hiyo iendelee au la.

Mbali na Mashinji na Matiko, washitakiwa wengine ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba John Mnyika, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13 likiwemo la kula njama, ambapo wote wanadaiwa kuwa Februari Mosi na 16, mwaka jana Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Chanzo: Habari Leo
Mahakama kuamua kesi vigogo 9 Chadema Mahakama kuamua kesi vigogo 9 Chadema Reviewed by Zero Degree on 9/25/2019 07:10:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.