Loading...

Mtoto wa Jenerali Mabeyo alijitabiria kifo


KIFO cha Nelson Mabeyo, mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance Mabeyo, aliyekuwa rubani wa ndege mali ya Kampuni ya Auric Air iliyoanguka juzi na kusababisha mauti yake kimezua simanzi, baada ya kuwepo kwa mazingira kama ya kijana huyo alijitabia kifo chake.

Aidha familia hiyo pamoja na uongozi wa kampuni ya Auric, wameeleza kuwa Nelson (24) alikuwa mbioni kwenda Canada mwezi ujao, kupata mafunzo ya kuendesha ndege aina ya Bombadier Q-400 chini ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL).

Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Habari leo hili jana, kaka wa marehemu, Denis Mabeyo alisema kifo cha Nelson aliyepoteza maisha na rubani pacha mwenzake, Nelson Olotu kimeacha pigo kubwa katika familia yao.

“Tumempoteza mtu aliyetosha katika maeneo yote, kwetu licha ya umri wake mdogo tulimheshimu kwa mawazo yake mazuri, alipenda kufanya kitu kipya kila siku kwa ajili ya kuyainua maisha yake, hakuwahi kuwa mtu wa kujikweza mbele ya wengine siku na wakati wote wa uhai wa maisha yake” alisema Denis.

Alisema Jumapili iliyopita, ambayo kwao kama familia ilikuwa siku ya mwisho kuonana naye, alitumia muda mwingi kukaa na kuzungumza na ndugu zake mambo mbalimbali na kufurahi nayo, bila ya wao kujua kuwa ndiyo alikuwa akiwaaga kabla ya kupatwa na ajali, iliyokatisha ndoto za maisha yake.

“Mimi nilikuwa Lebanon nimerudi hapa nchini Jumapili, sikupata hata nafasi ya kukutana naye kutokana na mizunguko yake ya kazi, zaidi tulikuwa tukiwasiliana katika simu tangu nilipofika, akiahidi kuwa angerudi katika safari hiyo na kuniona, lakini kumbe Mungu naye alikuwa amepanga lake, kifo cha mdogo wango ukweli kimeniumiza sana,” aliongeza Denis.

Baba Mdogo wa marehemu, William Mabeyo, alimtaja Nelson kuwa ni kijana aliyekuwa na uwezo wa kipekee na alikuwa na ndoto ya kuwa rubani wa ndege kubwa na kwamba mpango wa safari yake ya kwenda kujifunza kuendesha ndege ya Bombadier mwezi ujao nchini Canada, ndiyo mwendelezo wa mkakati wa kutimiza ndoto zake za kimaisha.

Kwa upande wake, Ofisa Operesheni wa Kampuni ya Auric Aira aliyokuwa akifanyia kazi Nelson, Rojoice Rukyaa na rubani wa kampuni hiyo, Kassim Ngayahiko walimtaja marehemu kuwa ni mchapakazi ambaye kampuni hiyo ilijivunia kuwa naye wakati wote.

Rukyaa alisema katika kipindi chote tangu ajiunge na kampuni hiyo mwaka 2016 akiwa kama mwanafunzi, uwezo wake uliendelea kukua kila siku hadi mwaka 2017 alipoanza rasmi kurusha ndege kama rubani aliyekidhi vigezo vyote vya kumfanya kurusha chombo cha aina hiyo angani.

Alisema hata alipokuwa akifanya kazi chini ya uangalizi, marubani wengi akiwemo Ngayahiko, walilidhishwa na kufurahishwa kutokana na uelewa wake wa haraka.

Pia wanamsifu kwa namna alivyokuwa na ushirikiano na wafanyakazi wenzake kipindi chote alichokuwa akifanya kazi mahali hapo.

Akizungumzia kuhusu taratibu za msiba huo, kaka wa marehemu alisema leo kuanzia saa nne, kutakuwa na misa ya kumuombea marehemu, itakayoendana na shughuli ya kuuaga mwili na baadaye kuanza safari kuelekea Kijiji cha Masanzakuona, Busega mkoani Simiyu kwa ajili ya kumpumzisha katika nyumba yake ya milele. Shughuli hiyo itafanyika kesho.
Mtoto wa Jenerali Mabeyo alijitabiria kifo Mtoto wa Jenerali Mabeyo alijitabiria kifo Reviewed by Zero Degree on 9/25/2019 08:05:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.