Mzamiru: Mara zote dabi ni mchezo mgumu
KIUNGO mkabaji wa Simba, Mzamiru Yassin amefunguka siri ya ubora alionao sasa ndani ya timu yake kuwa ni kurudia kutazama mechi alizocheza ili kutambua makosa yake asiyarudie mechi inayofuata.
Mzamiru amekuwa chaguo la kwanza chini ya Kaimu kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda tangu amepewa timu hiyo akichukua nafasi ya Zoran Maki aliyetimkia Misri.
Mzamiru alisema hajabahatisha kuingia kikosini moja kwa moja ni juhudi zake binafsi sambamba na kutumia vyema nafasi ambayo amekuwa akipewa huku akikiri kuwa Simba na Yanga ukiaminiwa unatakiwa kuwaaminisha kuwa hawajakosea kumpa nafasi.
“Nafurahi kuwa sehemu ya wachezaji wa kikosi cha kwanza haya ni malengo ya kila mchezaji kwenye timu yake kwani wanasajiliwa wachezaji wengi hatuwezi kucheza wote wanaotakiwa kucheza ni 11 tu hivyo juhudi binafsi za mchezaji ndio siri ya kuweza kupata namba,” alisema na kuongeza;
“Wachezaji wote waliopo Simba ni bora tunatofautiana namna ya kucheza hivyo kila mchezaji anatakiwa kupambana kumshawishi kocha kwenye uwanja wa mazoezi ili waweze kupata nafasi ya kucheza kama ilivyo kwa upande wangu.”
Akizungumzia mchezo kwa ujumla Mzamiru alisema; “Mara zote dabi ni mchezo mgumu kwasababu wachezaji tunacheza kwa presha kubwa kila mchezaji anataka kuonyesha nini alichonacho, tumeyapokea matokeo tunajipanga na michezo mingine iliyobaki.”
Simba itaivaa Azam kesho Alhamisi.