Serikali kukabiliana na changamoto ya wizi wa maudhui
Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma, alisema hayo katika hafla ya kuadhimisha mafanikio ya uzalishaji wa maudhui ya kitanzania unaofanywa na MultiChoice Tanzania iliyofanyika jijini, Dar es Salaam hivi karibuni.
Mwinjuma alisema serikali inaongeza nguvu katika kupambana na uvunjwaji wa hakimiliki na ndiyo sababu imeendelea kuiimarisha Ofisi ya Hakimiliki nchini (COSOTA), kwa kuiongezea vitendea kazi.
“Tutaendelea kushirikiana na mamlaka nyingine katika kuhakikisha suala hili linashughulikiwa kwa uzito unaostahili na katika hili tutahakikisha tunalishughulikia kwa muktadha mpana kwa sababu suala hili haliwaathiri wazalishaji wa maudhui tu, bali hata msanii mmoja mmoja,” alisema kiongozi huyo.
Aliipongeza MultiChoice Tanzania kwa uwekezaji mkubwa inayofanya katika uzalishaji wa maudhui ya ndani hususani filamu huku akiutaja uwekezaji huo kama chachu kubwa ya ukuaji wa tasnia ya filamu hapa nchini.
Alisema kitendo cha MultiChoice kuwa na chaneli maalum za Maisha Magic Poa na Maisha Magic Bongo ambazo hurusha maudhui ya Kitanzania, kumeifanya tasnia ya filamu kukua hapa nchini na kuongeza mchango wake katika kutoa ajira na kukuza uchumi.
Naye Mwenyekiti wa MultiChoice Tanzania, Balozi Ami Mpungwe, alisema kampuni hiyo imejipanga kuendelea kuwekeza katika uzalishaji wa maudhui ya kitanzania na ili kuhakikisha tasnia ya filamu inakua na inatoa mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi.
Chanzo: Nipashe
Serikali kukabiliana na changamoto ya wizi wa maudhui
Reviewed by Zero Degree
on
4/12/2024 09:05:00 AM
Rating:
