Loading...

CRDB yakabidhi pikipiki 20 kwa mkoa wa Arusha

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda.

Benki ya CRDB imekabidhi pikipiki 20 zenye thamani ya sh milioni 150 kwa mkoa wa Arusha kwa lengo la kuimarisha usalama katika mji huo wa kitalii.

Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, AbdulMajid Nsekela, alisema msaada huo ni matokeo ya kutenga asilimia moja ya faida anayoipats kila mwaka kwa ajili ya kurejesha kwa jamii katika sekta ya elimu na afya.

Alisema kila mwaka benki hiyo imekuwa ikifanya mikutano ikitanguliwa na mkutano wa wanahisa ambao huenda sanjari na kushiriki shughuli za kijamii ikiwemo kukabidhi madawati ikiwa ni mpango wa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan.

"Leo hii tupo Arusha tunafanya mkutano wetu wa 29 pia tutafanya makabidhiano ya pikipiki 20 kwa mkoa wa Arusha kwa ajili ya kuimarisha usalama na kukuza sekta ya utalii ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais wetu katika sekta ya utalii"alisema.

Aidha, Nsekela alielezea jinsi Benki hiyo ya CRDB inavyokuwa mstari wa mbele kupitia sera yao ya uwekezaji kwenye jamii na kumhakikishia kuwa uwekezaji huu unaolenga kwenye sekta ya afya, mazingira, elimu, vijana na wanawake unafanyika nchi nzima ikiwa ni sehemu ya mchango wa benki huyo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, aliishukuru benki ya CRDB kwa kuunga mkono adhma ya mkoa huo ya kuhakikisha kuwa usalama upo wakati wote ikiwa ni sehemu ya kuchagiza ukuaji wa utalii.

Alisema nyenzo hizo walizokabidhiwa leo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa katika kuimarisha doria maeneo mbalimbali ili kuhakikisha watalii wanaotembelea Arusha wanabaki salama mpaka muda wao wa kuondoka .

Aliwaonya wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwani jeshi la polisi lipo macho na watashughulikiwa kikamilifu.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, aliishukuru benki ya CRDB kwa msaada huo na kwamba wapo macho kuhakikisha wanalinda raia na mali zao usiku na mchana ikiwemo watalii wanaotembelea Mji wa Arusha.

Chanzo: Nipashe
CRDB yakabidhi pikipiki 20 kwa mkoa wa Arusha CRDB yakabidhi pikipiki 20 kwa mkoa wa Arusha Reviewed by Zero Degree on 5/17/2024 03:28:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.