Loading...

Filamu ya Royal Tour yazidi kuleta neema katika utalii


Filamu ya The Royal Tour iliyochezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuhamasisha utalii nchini, imeanza kuleta matokeo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha baada ya wawekezaji kuanza kujitokeza kwa lengo la kuwekeza kwenye miundombinu ya utalii.

Kampuni ya Six Rivers yenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa kampuni zilizojitokeza kuwekeza ndani ya hifadhi hiyo hasa kwenye ujenzi wa miundombinu inayochochea utalii pamoja na kushiriki kwenye shughuli za uhifadhi.

Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, Operesheni ya Kampuni hiyo ya Six River, Abubakari Mure, alisema kampuni hiyo imeanza kujenga uwanja wa ndege na maegesho ya ndege ndani ya hifadhi hiyo.

Alisema vilevile kampuni hiyo inajenga Chuo cha Utalii nje kidogo ya hifadhi hiyo katika Kijiji cha Mlungu kilichopo Kata ya Miyombweni ambacho kitasaidia vijana wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kupata maarifa ya utalii.

Alisema kampuni hiyo inakusudia kutumia Dola za Marekani milioni 1.1 kwenye uwekezaji wa awali ambapo uwanja utajengwa kwa Dola za Marekani 350,000 na ujenzi wa chuo utagharimu Dola za Marekani 750,000.

“Lakini tunakusudia kununua ndege mbili za doria ambazo gharama zake bado tunafuatilia, lakini huu uwanja wa ndege utakuwa na maegesho yenye uwezo wa kuegeshwa ndege mbili ndogo na helikopta moja,” alisema Mure.

Alisema uwekezaji huo unalenga kuchochea utalii katika hifadhi hiyo pamoja na hifadhi zingine za mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na kuwafundisha wananchi umuhimu wa uhifadhi.

Mwakilishi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Muhsin Mchau, alisema uwekezaji huo utasaidia kuboresha mazingira ya utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kwamba ndiyo maana walikubali na kuiruhusu kampuni hiyo kujenga uwanja ndani ya hifadhi.

Alisema mbali na uwanja huo pia chuo cha utalii kinachojengwa kitasaidia kutoa mafunzo kwa vijana wanaotokea mazingira ya jirani na hifadhi hiyo wakiwamo wa kutoka katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.

Alisema wananchi wengi wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini waliokuwa wanataka kuwasomesha watoto wao kwenye vyuo vya utalii walikuwa wanalazimika kuwapeleka mkoani Arusha ambako ndiko kwenye vyuo vingi.

“Uwekezaji huu utakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa maeneo haya, vijana watapata maarifa ya uhifadhi na kujua faida za uhifadhi, lakini pia idadi ya watalii itaongezeka na hivyo kuvutia wawekezaji wengine wakiwamo wa malazi,” alisema Mchau.

Vilevile alisema mazao ya wakulima wa maeneo ya jirani na hifadhi hiyo yatapata soko la moja kwa moja kutoka kwa wawekezaji ikiwamo chuo hicho cha utalii.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Homera aliwataka wawekezaji hao kufikiria pia kujenga kambi maalumu kwa ajili ya wageni watakaokuwa wanatembelea hifadhi hiyo kupumzika kabla ya kuelekea maeneo mengine.

Alisema uwekezaji huo pia utasaidia kuongeza ulinzi wa maliasili zilizomo ndani ya hifadhi hiyo kutokana na uwepo wa ndege za doria pamoja na elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa maliasili hizo.
Filamu ya Royal Tour yazidi kuleta neema katika utalii Filamu ya Royal Tour yazidi kuleta neema katika utalii Reviewed by Zero Degree on 6/12/2024 08:30:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.