Loading...

Mufti Mkuu ataka elimu ya ndoa


Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikhe Abubakari Zuberi amekabidhi Mpango Mkakati wa mmonyoko wa maadili kwa viongozi wa dini Mkoa wa Dodoma huku akitaka elimu kuhusu ndoa.

Mpango huo aliukabidhi Mei 16, 2024 kwa Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Rajabu, huku Naibu Kadhi Mkuu, Ally Ngeruko na Mwenyekiti wa Bakwata Taifa,  Hussein Mataka wakishuhudia.

Mkutano huo umehudhuriwa na Mashekhe wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma, walimu wa madarasa na jumuiya za vijana na wanawake za kiislamu wa mkoa huo.

Mufti Zuberi amesema bado kwenye jamii kunachangamoto ya kukosekana kwa elimu kuhusu ndoa hali ambayo imesababisha ndoa nyingi kuvunjika.

Amesema kupitia muongozo huo wataweza kuzuia uvunjikaji wa ndoa na jamii itakuwa na elimu kuhusu masuala ya ndoa.

Kwa upande wake Naibu Kadhi Sheikhe Ngeruko, amesema ndani ya mpango huo kuna kulinda misingi ya dini, kuimarisha umoja na amani, kuendeleza nidhamu, heshima na kukuza malezi bora.

Pia kuna kuinua ubora wa ibada, kupunguza migogoro na mzozo, kuimarisha uwajibikaji, kuchochea maendeleo ya jamii, kulinda sifa ya dini na msikiti na kujenga msingi wa jamii dhabiti.

Amesema lengo la kuunda mpango huo ni kutoa elimu ya kisheria, kupunguza mmonyoko wa maadili, kuimarisha usuluhishi na upatanishi, kukuza ushirikiano na madrasa.

Pia, kutoa muongozo wa maadili, kuwajengea uwezo viongozi wa kata, kutoa mafunzo kwa viongozi wa dini, kusimamia semina na kozi ili kuunda jamii yenye maadili thabiti.

Aidha, Naibu Kadhi huyo amesema zaidi ya asilimia 70 ya wana ndoa hawana elimu kuhusu ndoa hali ambayo imekuwa ikisababisha migogoro.

Amesema hali hiyo imesababisha baadhi ya watoto kukosa malezi ya pande mbili.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bakwata Taifa, Sheike Mataka amesema bado kuna changamoto ya mmomonyoko wa maadili na katika jamii watu hawalei.

“Talaka zimekuwa kama njugu, kila mmoja analalamika kuhusu masuala ya maadili Bakwata tumeona tunatakiwa kufanya jambo juu ya jambo hilo,” amesema Sheike Mataka.

Kwa upande wake Sheikhe wa Mkoa wa Dodoma, Rajabu amesema wamepokea miongozo hiyo na wataifanyia kazi.

“Viongozi wangu nami nimeanza kazi hapa hapa miongozo hii nimekabidhi kwa viongozi wangu Sasa kinachofuata ni utekelezaji tu,” amesema Sheikhe Rajabu.
Mufti Mkuu ataka elimu ya ndoa Mufti Mkuu ataka elimu ya ndoa Reviewed by Zero Degree on 5/18/2024 07:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.