Loading...

Pambano la Mwakinyo lafutwa


Kamisheni ya ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) imesema, haijaidhinisha kufanyika pambano la ngumi kati ya bondia Mtanzania Hassan Mwakinyo dhidi ya Patrick Allotey kutoka Ghana.

Pambano hilo la kimataifa lilipangwa kufanyika Mei 31 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya mpito ya Kamisheni hiyo, Alex Galinoma, alisema wamefanya uamuzi huo kutokana na uvunjaji wa mikataba, ukiukwaji wa vigezo na masharti uliofanywa na mwandaaji wa pambano hilo, Shomari Kimbau kupitia kampuni yake ya ‘Golden Boy Promotion Inc’, jambo ambalo wamelielezea kuwa linauchafua mchezo huo.

Aidha aliweka wazi kuwa uvunjaji wa vigezo na masharti hayo kuwa ni pamoja uwasilishaji usiokamilika wa nyaraka zinazohitajika, ikiwamo mikataba kamili ya mabondia, rekodi za matibabu na vibali vya tukio hilo.

"Tumeamua kuchukua uamuzi huu wa kutolitambua pambano hilo baada ya kubaini muandaaji wa pambano hilo kutotimiza matakwa ya kufanyika pambano hilo, hajatoa maelezo ya fedha za kuwalipa mabondia pamoja na malipo ya ada ya kufanya pambano hilo,” alisema Galinoma.

Aidha, aliongeza kuwa mwandaaji huyo ameshindwa kupata ukumbi unaofaa kufanyika kwa pambano hilo ndani ya muda uliokubaliwa na kuwasilisha nyaraka kuonyesha kupatikana kwa ukumbi huo.

Galinoma, alisema mwandaaji ameshindwa kuwa na mawasiliano na ushirikiano mzuri na tume hiyo kulikopelekea mambo mengi kutokamilika kwa wakati.

Mwandaaji wa pambano hilo, Kimbau hakupatikana kutolea ufafanuzi wa maamuzi hayo licha ya juhudi za kumtafuta.
Pambano la Mwakinyo lafutwa Pambano la Mwakinyo lafutwa Reviewed by Zero Degree on 5/30/2024 06:02:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.